×

Magufuli: Wanasiasa Msichokoze Vyombo vya Dola

RAIS John  Magufuli amevitaka vyama vyote vya siasa kufanya kampeni za staha na kuheshimu sheria za nchi, sheria na taratibu za uchaguzi ili uwe wa huru na amani.

 

Magufuli amesema hayo leo, tarehe 22, Julai 2020, wakati akizinduwa Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ( NEC) eneo la Njedengwa jijini Dodoma ambalo limegharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 16.8 zilizookolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

 

“Tufanye kampeni zetu kwa kujenga umoja wa taifa letu Tanzania, tunadi sera zetu na wananchi waweze kutupima kutokana na sera zetu, wasitupime kwa ajili ya matusi tunayo tukanana. Huu ndiyo wakati wa kujinadi. Baada ya uchaguzi siasa zinabaki bungeni, atakayeshinda anaingia kwenye kazi.

 

”Niviombe vyombo vya dola vituvumilie kidogo, ila visitumie nguvu, na sisi wanasiasa tusifanye mambo ambayo yatavifanya vyombo ya ulinzi vitumie nguvu, niwaombe na wanasiasa, msivichokoze vyombo vya ulinzi na usalama, msivifanye vitumie nguvu sehemu ambazo haihitajiki, nawasihi tufanye kampeni za staha, tumtangulize Mungu mbele.

 

“Kwa sasa ni ruksa kila mmoja akafanye kampeni zake kwa kadri ratiba itakavyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Kila mmoja afanye kampeni kwa uhuru, kwa uwazi na akafanye vizuri akimtumaini Mungu. Narudia kuhimiza vyama vya siasa kushirikiana katika uchaguzi huu na kujiepusha na vitendo vya vurugu. Vurugu hazijengi, zinabomoa,” amesema Magufuli.

Leave a Comment