
MAJIBIZANO ya mchekeshaji Idris Sultan na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ yameibua mazito, yamefukua makaburi.
NI MWENDELEZO WA CHUKI
Zari ambaye ni mzazi mwenza wa mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, kupitia majibizano hayo, anadaiwa kufufua ile skendo ya uchawi ya mwanamitindo Hamisa Mobeto ambaye naye amezaa na Diamond au Mondi.
Zari anaendelea kuonesha chuki ya waziwazi dhidi ya Mobeto ambaye anaamini ndiye aliyesababisha kutengana na Mondi baada ya kuchepuka na kuzaa naye.
KWANI ILIKUWAJE?
Ilikuwa hivi; Idris aliweka picha ya mwanamke mwenye shepu matata akiwa amechuchumaa na mwanaye na kuonesha anavyochati na baba wa mtoto ili apate pesa za matumizi.
Kwenye picha hiyo, Idris alisindikiza na maneno; “Michezo ya Zari.”
Muda mfupi baadaye Zari aliibuka na kumjibu Idris kwenye picha hiyo; “Unamjua wa kumtagi sema unaogopa uchawi.”
Kwa mujibu wa Idris, Zari anaonekana huwa anatumia staili na pozi hilo la picha anapohitaji matunzo ya watoto wawili kutoka kwa Mondi na inaonekana ndiyo staili aliyotumia kumshawishi jamaa huyo akamuongezea pesa za kununua gari la kifahari aina ya Bently hivi karibuni.
WAFUASI WA MOBETO…
Maneno hayo ya Zari, yaliamsha hasira za wafuasi wa Mobeto ambao walidai kuwa, alimlenga mwanamitindo huyo ilhali hakuwa ametaja jina la mtu.
Walisema, Zari alimlenga Mobeto kwa sababu ya ile skendo iliyowahi kumbamba akihusishwa na mambo ya uchawi.
Kwa muda mrefu Zari na Mobeto hawajawahi kuwa na mazungumzo mazuri ama kwa mmoja kumtaja mwingine kwa baya au zuri, hivyo Zari ameonekana kuuwasha moto uliokuwa umebaki majivu.
TUHUMA ZA UCHAWI
Wafuasi hao walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, Zari anaendeleza tuhuma za uchawi dhidi ya Mobeto ambazo ziliwahi kuibuliwa na mama mzazi wa Mondi, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’.
Katika tuhuma za Mama Dangote, Mobeto alidaiwa kwenda kwa mganga ili kumuweka Mondi kwenye himaya yake.
Mondi pia aliwahi kugusia ishu hiyo kwenye moja ya ngoma zake akiimba; “Tunguli limenibamba!” Akimaanisha uchawi ulikuwa umemkamata kisawasawa.
Majibizano hayo ya Idris na Zari, yalikuja muda mfupi baada ya Mondi kupigia debe (promo) mavazi anayouza Mobeto kuonesha kuna ukaribu fulani wa kusapotiana katika kazi zao, jambo ambalo linadaiwa kumfanya Zari alipuke.
MONDI AWAPA MWALIKO MA-EX WAKE
Hata hivyo, katika kuonesha kwamba hana tatizo na wanawake wake wa zamani (ma-ex), Mondi alimpa mwaliko Zari, Mobeto na Wema Sepetu wa kuhudhuria shoo ya mwanamuziki wake, Zuchu iliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar.
MOBETO: UMBEYA SITAKI
Kama ilivyo desturi yake, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA huwa haliwezi kukaa na ukakasi kooni, hivyo limemtafuta Mobeto ili kusikia anasemaje juu ya ishu hiyo.
Mobeto amesema kwa sasa amebadilisha mfumo wa maisha yake moja kwa moja, ndiyo maana siku hizi yupo dukani kwake (Kijitonyama jijini Dar) saa zote na hana muda wa kujibizana na watu.
Amesema kwa sasa maisha yamebadilika na kila mtu anatakiwa kufikiria ni kitu gani cha kufanya ili watoto wale, wasome vizuri na siyo kuwa bize na maisha ya watu wengine, kwani siyo sawa kwa upande wake.
“Maisha yangu ya sasa siyo yale ya miaka miwili au mitatu iliyopita. Niko bize dukani kwangu (Mobetto Style Boutique) kuanzia asubuhi hadi jioni na kwa kweli ndiyo maisha ninayoyaona yenye maana zaidi kuliko maisha mengine ya kumfuatilia mtu au kufanya vitu ambavyo sivyo kabisa,” amesema Mobeto ambaye kwa sasa anaongoza kwa kushona madera na nguo mbalimbali.
STORI: IMELDA MTEMA, DAR