WANAKIJIJI wa Lupaso na vijiji jirani wanaendelea na kusafisha mazingira ya makazi yao wakijitayarisha kuupokea mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye atazikwa huko.
Matayarisho hayo ni pamoja na kuwka mazingira safi kwa kupokea wageni mbalimbali watakaofika kwa ajili ya shughuli za kuuaga mwili huo na maziko.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuanzia kesho Jumapili, Watanzania watapata fursa ya kushiriki shughuli za kuuaga mwili wa Mkapa zitakazofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, shughuli ambazo zitafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe Julai 26 hadi 28.
Siku ya Jumapili kuanzia saa nne asubuhi, Kanisa Katoliki litaongoza misa ambayo wakazi wa Dar es Salaam na nje ya mji huo watapata fursa ya kuuaga mwili huo baada ya misa ambapo zoezi hilo litaendelea mpaka Jumatatu.

Jumanne, Julai 28 itakuwa siku ya kuuaga kitaifa kwa viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini na wananchi. Baada ya zoezi hilo majira ya alasiri mwili wake utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara kwa maziko.
Baada ya kutua uwanja wa ndege wa Nachingwea patakuwa na fursa kwa wakazi wa eneo hilo kuuaga mwili huo ambao utapumzishwa Jumatano Julai 29, 2020, saa 8 mchana katika kijiji hicho cha Lupaso.
CREDIT: EATV