×

Kaburi la Mkapa Laanza Kuandaliwa

ASKARI wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wameanza kuchimba kaburi linalotarajiwa kutumika kuupumzisha mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia jana Julai 24, 2020. Rais Mkapa anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa jana alisema kuanzia kesho Jumapili, Watanzania wote watapata fursa ya kushiriki shughuli za kuaga zitakazofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Shughuli za kuaga   zitafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 26 mpaka tarehe 28, kuanzia Jumapili mpaka Jumanne.

Siku ya Jumapili kuanzia saa nne asubuhi, Kanisa Katoliki litaongoza misa ambayo wakazi wa Dar es Salaam na nje ya mji huo watapata fursa ya kuaga mwili baada ya misa, na zoezi hilo litaendelea siku nzima mpaka siku ya Jumatatu siku nzima pia itatumika kwa shughuli hiyo.

Jumanne, Julai 28 itakuwa siku ya kuaga kitaifa ambapo viongozi mbalimbali wa serikali nchini, viongozi wa dini, na wananchi. Baada ya zoezi hilo majira ya alasiri mwili wake utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara kwa mazishi.

Utatua katika uwanja wa ndege wa Nachingwea na kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo kuaga mwili wa marehemu na kupumzishwa Siku ya Jumatano Julai 29, 2020, saa 8 mchana katika Kijiji cha Lupaso.

CREDIT: EATV & AZAM TV

 

 

Leave a Comment