
NAELEZWA uongozi wa timu ya Simba umeshamalizana na aliyekuwa mshambuliaji wa Rayon Sport ya Rwanda, Mghana, Michael Sarpong.
Simba imekamilisha usajili wa mshambuliaji huyo aliyeanza kuwindwa na Yanga kabla ya Simba kuingilia kati na kumalizana naye fasta.
Taarifa za uhakika ambazo Spoti Xtra, limezipata kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshakamilisha asilimia 80 ya usajili huo na kinachosubiriwa kwa sasa ni kumaliza mchezo wa fainali ya Kombe la FA ili mchezaji huyo kuanzia wiki ijayo atue kusaini mkataba.

“Sarpong ameshamalizana na Simba kila kitu isipokuwa bado vitu vichache ambavyo vitakamilishwa atakapokuwa ameingia nchini, baada ya Simba kucheza fainali ya FA ndiyo itajulikana lini anakuja.
“Unajua wao wanaongea na meneja wake na ndiye anasimamia kila kitu, hivyo baada ya mchezo huo wa FA ndiyo kila kitu kitafahamika kwani kwa sasa akili yao yote ipo kwenye mchezo huo,” kilieleza chanzo.
Spoti Xtra, lilimtafuta meneja wa mshambuliaji huyo, Mnyarwanda, Alex Kamanzi, ambaye alisema wameshakubaliana na Simba kila kitu na kwa sasa wanasubiri ni lini wataambiwa waje nchini kukamilisha dili hilo.

“Kila kitu kinaenda sawa katika makubaliano yetu isipokuwa kuna mambo machache ambayo nadhani yatakuja kukamilikia huko kwa sababu tunasubiri watume tiketi ili tuweze kufika,” alisema Kamanzi.
Hivi karibuni, chanzo chetu kilieleza kwamba, mshambuliaji huyo baada ya kukubaliana kila kitu na Simba, ameandaliwa mkataba wa miaka miwili huku dau lake likiwa ni dola 60,000 (zaidi ya Sh milioni 138)
STORI: IBRAHIM MUSSA, DAR