×

Rais Magufuli Ayaanika Maajabu ya Mkapa – Video

 

RAIS John Magufuli ameanika mambo makubwa aliyoyafanya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin William Mkapa wakati wa utawala wake na utumishi wake ndani ya Serikali ya Tanzania.

 

Amesema hayo leo, Julai 28, 2020, wakati akihutubia waombolezaji na Watanzania wote katika Uwanja wa Uhuru kwenye zoezi la kuaga kitaifa mwili wa Mkapa kabla ya kupelekwa nyumbani kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara, ambako anatarajiwa kuzikwa kesho.

Baadhi ya kauli alizotoa Rais Magufuli zinafuata hapa chini:

“Julai 23, taifa letu lilipatwa na pigo kubwa la kuondokewa na aliyekuwa Rais wetu wa awamu wa Tatu, kifo chake kimeacha majonzi na simanzi kubwa, siyo kwa familia yake na nchi yetu lakini katika eneo letu la Afrika Mashariki na Dunia kiujumla.

 

“Kwa niaba ya Serikali pamoja na Watanzania wote napenda kutoa salamu za pole kwa Mama Anna Mkapa kwa kuondokewa na mume wake mpenzi, watoto wake na wajukuu kwa kuondokewa na babu yao;  napenda niwahakikishie wanafamilia wote kwamba tupo pamoja nanyi.

 

“Tangu msiba huu umetokea watu wengi wamejitokeza na kumuelezea, kama nyote mjuavyo, amefariki dunia ikiwa imepita miezi minane tu tangu azindue kitabu cha chake cha ‘My Life, My Purpose’, ndani ya kitabu hicho ameandika kwa urefu sana historia ya maisha yeke.

 

“Mzee Mkapa aliikuta nchi ikiwa na madeni akapambana na nchi ikasamehewa deni la USD bilioni 3 kati ya USD bilioni 7 katika mpango ambao ulisimamiwa na Benki ya Dunia na IMF, Mzee Mkapa aliamini pia kuwa nchi inapaswa kujitegemea licha ya kusamehewa deni.

 

“Mzee Mkapa aliwapenda Watanzania hususani wanyonge ndiyo maana alifuta kodi ya kichwa, kodi ya mifugo na kodi ya baiskeli ambazo ziliwatesa sana watu, ilikuwa ikisababisha hata watu kukimbia makazi yao, hii yote inadhihirisha jinsi Mzee Mkapa alivyokuwa anapenda watu.

 

“Alianzisha MKURABITA na TASAF kusaidia kaya masikini. Nawapa pole Mama Anna Mkapa, watoto wake, na wajukuu kwa kuondokewa na mpendwa wetu. Lakini pia nachukua nafasi hii kutoa pole kwa Watanzania wote.

 

“Mzee Mkapa alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu mwaka 1995, katika uchaguzi wa kwanza uliohusisha vyama vingi, hii ina maana kuwa Mzee Mkapa ni baba wa demokrasia nchini. Mkapa ni baba wa demokrasia nchini, hata utaratibu wa kutoa ruzuku kwa vyama vya siasa yeye ndiye aliuanzisha.

 

Katika utawala wa Mzee Mkapa ndipo Taasisi ya Kuzuia Rushwa PCB (sasa TAKUKURU), ambapo sasa inaitwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Yeye ndiye alikuwa wa kwanza kuanzisha wizara maalum ya kushughulikia masuala ya utawala bora na mara baada ya kuingia madarakani Mzee Mkapa aliahidi serikali yake ingejengwa katika misingi ya ukweli na uwazi na kwamba asingekuwa na huruma kwa wala rushwa.

 

“Rais Mkapa amefariki ikiwa ni miezi michache tangu alipotoa kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ ambapo ameelezea mambo mengi ikiwemo maisha yake na uongozi tangu akiwa Lupaso. Watanzani watamkumbuka Mzee Mkapa kwa mengi ikiwemo mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya, ikumbukwe alikuta nchi ikiwa na madeni makubwa.

 

“Mzee Mkapa alianzisha TRA na kuongeza mapato ya nchi, aliongeza akiba ya kigeni, alipunguza mfumuko wa bei pia kwa ujumla mafanikio mengi ya kiuchumi tunayoyashuhudia sasa dira yake ilianzia wakati wa uongozi wa Mzee Mkapa.

 

“Alianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES), pia alianzisha mpango wa elimu kwa waliokosa kusoma (MEMKWA), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, NECTA, TCU na kuifanya VETA kuwa taasisi inayojitegemea.

 

“Kifo cha ais mstaafu Mkapa kimeacha majonzi, siyo kwa familia na taifa letu, bali pia katika nchi za Afrika Mashariki, Afrika na dunia nzima. Watanzania wengi wanamkumbuka Mzee Benjamin Mkapa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya.”

 

Leave a Comment