
RAIS John Magufuli ameonyesha kukereka na kitendo cha kukuta kilometa 90 za Barabara ya lami YA Kilwa – Somanga Ikiwa imeharibika vibaya huku Wizara ya Ujenzi na TANROADS wakichelewa kushughulikia barabara hiyo muhimu.
Tukio hilo limetokea leo Alhamisi, Julai 30, 2020, wakati Magufuli akizungumza na wananchi hao alipokuwa njiani akirejea jijini Dar es Salaam akitokea Lupaso, Masasi mkoani Mtwara kwenye mazishi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa ambaye alizikwa jana.
“Ilibidi niende Dar es Salaam kwa kutumia ndege kutokea Mtwara lakini nimepita hii barabara (Lindi – Dar) makusudi nione hali yake, magari yenye uzito mkubwa yameharibu hii barabara.
“Huwezi ukaamini kama tuna Waziri wa Ujenzi au Naibu Waziri wa Ujenzi au Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi; kilometa zote 90 nilikuwa nahesabu zimeharibika.
“Kwa mujibu wa sheria ya barabara, barabara ikiwa ya lami inapata 100% ya ukarabati. Fedha za Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund) sijui zinakwenda wapi! Tunatuma fedha za Bodi ya Mfuko na fedha za halmashauri, haiwezekani barabara iwe mbovu. Hakuna stendi Somanga.
“Mmeniudhi Wizara ya Ujenzi, sijafurahia, nimetoka na machungu kwa kumzika Mzee Mkapa, lakini hapa Somanga napo nimepata machungu kwa kukuta barabara hii haijatengenezwa hata visehemu vidogo vidogo, niachieni nitalishughulikia,” amesema Rais Magufuli.