
KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya soka ya Polisi Tanzania, Marcel Kaheza, amesema kwamba kila kitu kuhusu ishu yake ya kusaini Yanga kimekamilika na anachosubiri kwa sasa ni simu kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo ambao wameahidi kumwita ili amwage wino.
Kaheza ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu baada ya kuhusika kwenye mabao 12 ya Polisi Tanzania, amefunga mabao saba na kuasisti mengine matano.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kaheza alisema ni kweli Yanga wamepeleka ofa mezani na kilichobaki kwa sasa ni simu yao tu ili akamwage wino.
“Nimeongea na meneja wangu ambaye ameniambia kuwa Yanga imeleta ofa na mazungumzo yamefikia katika hatua nzuri ishu iliyobaki kwa sasa ni kusubiri simu yao ili kwenda kukamilisha taratibu za kusaini rasmi mkataba,” alisema Kaheza.
Akisherehesha taarifa hiyo, Meneja wa Kaheza, Kally Ongala, alithibitisha kuwepo kwa ofa kutoka miongoni mwa klabu kubwa hapa nchini na mazungumzo yanaendelea vizuri.
“Ni kweli mezani kwetu kuna ofa tatu, moja ni ya klabu kutoka nje ya nchi na mbili ni za hapa nyumbani, miongoni mwa hizo mbili ofa moja inatoka kwenye klabu kubwa hapa nchini ambayo sipo tayari kuitaja kwa sasa.
“Lakini napenda watu wajue kuwa mazungumzo yanaenda vizuri na kama kila kitu kitaenda vizuri basi kila kitu kitawekwa wazi hivi karibuni,” alisema Ongala.