
KIUNGO mpya wa Azam, Ally Niyonzima, raia wa Rwanda, amefunguka kuwa ana furaha kubwa ya kufanikiwa kujiunga na timu hiyo huku akisisitiza kuwa kilichomleta nchini ni kufanya kazi kwa kuwa yeye ni mpambanaji.
Kiungo huyo aliyekuwa akiwindwa na Yanga pamoja na Simba, amejiunga na Azam kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sports ya nchini Rwanda.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Niyonzima alisema kuwa kitu kikubwa kilichomfanya kuja nchini ni kupiga kazi kwa kuwa yeye ni mchezaji wa kupambana.
“Kwanza nashukuru nipo hapa, japokuwa haikuwa kazi rahisi lakini kwa mapenzi ya Mungu nimekuwa kwenye familia ya Azam, nipo hapa kwa ajili ya suala moja nalo ni kazi kwa sababu mimi ni mchezaji wa kupambana na hiyo ndiyo imekuwa kitu kikubwa kichwani mwangu.
“Naamini nitakuwa msaada wa ndani ya timu kwa ushirikiano na wenzangu kuelekea kwenye msimu ujao, ushindani ni jambo la kawaida kwangu, halina shida kwa sababu soka ni kazi yangu, hivyo mashabiki wategemee mambo makubwa kutoka kwangu,” alisema Niyonzima.
IBRAHIM MUSSA NA JOEL THOMAS