
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhi rasmi ofisi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa Mpya wa Dar, Aboubakar Kunenge, leo Jumatatu, Agosti 3, 2020 katika ofisi hizo zilizopo Ilala, jijini Dar es Salaam.
Akizunumza wakati wa kukabidhi ofisi hiyo, Makonda amesema:
“Kazi ya uteuzi siyo rahisi ina taarifa na maelezo mengi, lakini Rais Magufuli aliamini katika vijana, nikiwa kijana wa kwanza kupewa majukumu katika mkoa mkubwa na kuacha alama itakayodumu milele yote. Ningekuwa ni jeshini ninazo medali za kivita ni askari mmoja aliyepo back bencher mwenye uwezo mkubwa wa kupigana vita yoyote.
“Kwa hiyo Mheshimiwa RC, Mambosasa na timu yenu mkihitaji uzoefu wangu katika mapambano ya kumlinda Dkt John Pombe Magufuli, hata kama ni saa tisa usiku nitaamka. Kwangu yeye ni zaidi ya cheo, ni baba.

“Nimshukuru sana mke wangu Maria na mwanangu kipenzi Keagan kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuvumilia masimango na maneno ya hovyo na machafu yaliyotamkwa juu yao na familia yangu katika kipindi chote cha utumishi wangu na yatakayoendelea.
“Nasema haya kwa sababu naaga, sitegemei tena kurudi katika nafasi hii kwenye ofisi hii, nikija hapa basi nitakuja kama mwananchi wa kawaida na nitapanga foleni pale. Na wala msisite na maneno ya watu ya kwamba ataishije, ataenda wapi, mngeumia zaidi siku mkisikia Makonda amemuacha Yesu, Lakini maadamu Yesu ninaye, msiwe na shaka na mimi maisha yangu yapo salama.