×

Miaka 22 Shambulio Ubalozi wa Marekani Dar, Nairobi

MWAKA 1998, Agosti 7, majira ya saa 4 asubuhi, siku ya Ijumaa katika mitaa ya Dar es Salaam na viunga vya jiji la Nairobi kulikuwa na patashika baada ya milipuko kutokea katika balozi za Marekani nchini Tanzania  na Kenya.

Jijini Dar es Salaam, asubuhi majira ya saa 4, gari lililobeba mabomu hayo liliendeshwa kupitia barabara ya Laibon ulipokuwepo Ubalozi wa Marekani kuelekea moja kati ya mageti mawili ya ubalozi huo na kulipuka majira ya 4 na dakika 39.

Ubalozi wa Marekani ulihamia katika majengo hayo ambayo yaliyokua ubalozi wa Israel, mnamo Mei 1980 ambayo yalijengwa miaka ya 1970. Pamoja na watu wa usalama wa ubalozi, ulinzi pia ulikuwa ukiimarishwa na kampuni ya Ulinzi ya Ultimate Security. Wakati huo hakukuwa na ulinzi wa polisi kama ilivyo sasa.

Takribani wiki mbili kabla ya milipuko hiyo, jijini Dar es Salaam afisa usalama wa kanda, John DiCarlo, aliwasili tarehe 22 Julai 1998 na kubadilisha utaratibu wa ukaguzi magari kuhakikisha magari yanakaguliwa nje kabla ya kuingia. Pamoja na hatua zingine ya kiusalama, ikiwemo mazoezi ya kutambua mabomu ya vifurushi yaliyofanyika dakika 30 kabla ya mlipuko, haikuweza kuzuia mlipuko wa Agosti 7.

Watu wawili walioendesha lori dogo lenye kilogramu 700 za baruti walifika mbele ya ubalozi wa Marekani uliokuwepo njia-panda ya barabara za Moi na Haile Selassie.. Dereva Azzam aliingia kwenye njia ya kutoka katika maegesho ya magari.

Hapa alizuiliwa na mlinzi Benson Okuku Bwaku aliyekataa kufungua geti ya gereji. Gaidi wa pili Mohamed Rashed Daoud Al-Owhali alimtupia kombora ya mkononi lakini alimkosea. Bwaku alifaulu kukimbia na kufikia kona ya jengo akajiokoa. Hapo Azzam alianza kufyatua risasi hovyo.

Hapo Al-Owhali alikimbia kuelekea mtaa wa Haile Selassie akajiokoa wakati Azzam akajilipua kwa baruti kwenye lori. Mlipuko mkubwa ulitikisisha ubalozi na jengo jirani la Ufundi Building.

Majengo ya ubalozi yaliharibiwa vibaya na kupelekea kutotumika tena, baadhi ya majengo ya karibu pia yaliharibiwa vibaya yakiwemo ya Balozi za Ufaransa na Ujerumani  lakini hakuna aliejeruhiwa.

Leo, Kenya na Tanzania zinafanya kumbukizi ya miaka 22 tangu kutokea kwa shambulizi hilo wakati baadhi ya waliofikwa na kadhia hiyo bado hawajafidiwa.

Takribani watu 224 waliuawa na kujeruhi  wengine zaidi ya 5,000, ikiwa ni pamoja na Balozi wa Marekani Prudence Bushnell. Watu 213 waliuawa katika Ubalozi wa Marekani Nairobi na watu 11 waliuawa katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi 44 wa ubalozi (Wamarekani 12 na watu 32 wa kigeni),

 

Vifo vingi vilitokea kwa sababu jengo dogo jirani la Ufundi Building lilibomolewa kabisa na kuanguka. Wahanga wengi walikuwa vijana wanafunzi waliosoma kwenye chuo cha ukarani ndani ya jengo hili pamoja na walimu na wafanyakazi wake.

 

Pamoja na watu waliojeruhiwa katika majengo ya karibu, kuna wengi waliouawa na kujeruhiwa kwenye barabara ya Haile Selassie kwa sababu moto na mshtuko wa bomu zilielekezwa kati ya kuta za ubalozi na Ufundi Building. Basi iliyokwama kwenye msongamano wa magari mbele ya kiingilio cha ubalozi ilichomwa kabisa pamoja na abiria zake.

 

Watu wengi walijeruhiwa macho kwa vipande vya kioo; walisikia mlipuko wa kwanza wa kombora la mkononi na risasi zilizofyatuliwa na Azzam wakaenda madirishani kuangalia kuna nini wakapigwa vipande vya kioo cha madirisha usoni wakati bomu ililipuka.

 

Marekani ilimshutmu mwana wa Saudi, Osama bin Laden, kuhusika na upangaji na utekelezaji wa milipuko hiyo. Kati ya waliohusika, wawili ni raia wa Tanzania. Khalfan Khamis Mohamed ambaye anatumikia kifungo katika gereza lenye ulinzi mkali ADX Florence.

Khalfan alikamatwa nchini South Africa na kisha kupelekwa Marekani siku iliyofuata. Kusafirishwa kwa Khalfan kutoka SA kwenda Marekani kulipekea kesi maarufu chini ya mahakama ya kikatiba Mohamed v President of the Republic of South Africa iliyoamua kuwa serikali ya SA haitofanya “extradition” kwa mtuhumiwa ambaye anaweza kuhukumiwa kifo bila ya kupata hakika kuwa mtuhumiwa huyo hatahukumiwa kifo.

Mshitakiwa wa pili ni, Ahmed Khalfan Ghailani pia mzaliwa wa Zanzibar, aliyekamatwa mwaka 2004 na shirika la Intelijensia la Pakistan na kisha kupelekwa Marekani. Alishikiliwa ndani ya Guantanamo Bay mpaka 2009 alipohukimwa kutumikia kifungo cha maisha katika gereza la McCreary mjini Kentucky, Marekani.

Baada ya shambulizi hilo, zaidi ya maafisa 900 kutoka FBI walipelekwa katika majiji hayo mawili kusaidia uchunguzi, kutafuta ushahidi na kutambua wahanga wa matukio hayo na kusaka watu waliofanya tukio hilo. Kwa mujibu wa mwandishi Lawrence Wright, katika kitabu chake “The Looming Tower: Al-Qaeda and the Road to 9/11” shambulio la Dar es Salaam lilipewa jina la “Operation al-Aqsa”

Jitihada za uchunguzi katika kubaini wahusika nchini Tanzania zilihusisha wachunguzi wa Kitanzania chini ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Adadi Rajab (Mbunge wa Muheza aliyemaliza muda wake) na wachunguzi wa Marekani kutembelea gereji moja huko Kimara iliyokuwa ikifahamika kama Tommy Spades Manufacturing ambayo wachunguzi walihisi ndipo mahala ambapo bomu lilitengenezwa na kisha kuchomelewa kwenye chesisi ya gari iliyotumika katika kulipua ubalozi huo.

Mpaka sasa zaidi ya watu 20 wamehukumiwa. Baadhi ya wahusika, akiwemo Osama bin Laden, wameuawa. Sita wanatumikia kifungo katika magereza nchini Marekani na wachache wanasubiri hukumu.

Operation Infinite Reach:
Bill Clinton (1993-2001) aliruhusu Marekani kujibu mashambulizi kwa kutupa makombora na kulipua ngome ya Al-Qaeda huko Khost Afghanistan na kiwanda kikubwa mjini  Khartoum nchini Sudan ambacho mmiliki wake alisadikika kuwa na uhusiano na kumsaidia kifedha Bin Laden.

 

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Namba 1189:

Umoja wa Mataifa kupitia baraza lake la usalama ulipitisha makubaliano kwa kauli moja ya kulaani vikali shambulio la kigaidi nchini Tanzania na Kenya.

 

Aprili, 2014 jaji katika mahakama ya Washington DC, Marekani,  alitoa uamuzi kwamba Watanzania na Wamarekani waliokufa au kujeruhiwa katika shambulizi la ubalozi jijini Dar es Salaam walipaswa kulipwa fidia ya Dola za Marekani 957 milioni.

 

Mwaka huohuo mahakama ya New York, iliwapa haki ya kulipwa Dola bilioni  1 raia wengine sita wa Kenya walioathirika na shambulizi la bomu jijini Nairobi. Hata hivyo, iliamuliwa kuwa fidia itapatikana baada ya kukamatwa na kutaifishwa mali kutoka kwa kundi la Al- Qaeda lililotuhumiwa kuhusika na mashambulizi hayo.

 

Waathirika wa milipuko hiyo ni 538 ambao ni raia wa Kenya, wanasema hata kama itawachukua miaka 30 kupata haki yao, hawatakata tamaa kupigania wanachoamini ni haki yao.

 

Mwanasheria anayewawakilisha watu hao, Philip Musolini, alinukuliwa Jumapili iliyopita na gazeti la Sunday Nation la Kenya akisema wameanza kuwasiliana na baadhi ya wabunge wa Bunge la Congress kushawishi kufanyika marekebisho ya sheria ya fidia iliyopitishwa mwaka 2015 inayotoa fidia kwa raia wa Marekani walioathirika kwenye mashambulizi.

 

Alisema licha ya Congress kutoonyesha ishara yoyote kwamba marekebisho yatafanyika hivi karibuni,  ana matumaini njia hiyo itazaa matunda.

 

 

Watu wafuatao walifunguliwa mashtaka na kuhukumiwa katika mahakama ya Shirikisho la Marekani kuhusiana na mashambulizi hayo:  
  • Mamdouh Mahmud Salim, mwanachama mwanzilishi wa al-Qaida, alikamatwa mnamo Septemba 1998 nchini Ujerumani na  anatumikia hukumu ya maisha katika jela ya shirikisho kwa kuhusika kwake.
  • Mnamo Oktoba 2001, viongozi wa al-Qaida, Wajh El-Hage, Khalfan Khamis Mohamed, Mohamed Rashed Daoud Al-Owhali, na Mohamed Sadeek Odeh walihukumiwa kwa kupanga na kutekeleza ulipuaji wa mabomu ubalozini na kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
  • Mnamo Januari 2011, kiongozi wa al-Qaida Ahmed Khalfan Ghailani alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha katika mahakama ya Marekani kwa kuhusika kwake  na mabomu hayo.
  • Mnamo Septemba 2014, Adel Abdel Bari, kiongozi wa karibu wa kiongozi wa al-Qaida, Zawahiri, alikubali kuwa na hatia ya kuua watu Wamerekani na kuhukumiwa  miaka 25 na mahakama ya shirikisho.
  • Mnamo Mei 2015, Khaled al-Fawwaz, naibu wa Usama Bin Laden, alihukumiwa kwenda jela na mahakama ya shirikisho kwa kuunganishwa kwake na mashambulizi hayo.
Watuhumiwa wafuatayo walifunguliwa mashtaka kwa mabomu na jopo kuu la shirikisho la Marekani:

 • Ayman al-Zawahiri, kiongozi wa sasa wa al-Qaida

• Sayf al-Adl, kiongozi muhimu wa al-Qai’da

• Abdullah Ahmed Abdullah, kiongozi muhimu wa Qai’da

• Usama bin Laden, kiongozi wa zamani wa al-Qaida (Marehemu)

• Mohammed Atef, kiongozi wa zamani wa kijeshi wa al-Qaida (Marehemu)

• Anas al-Libi, kiongozi wa zamani wa al-Qaida (Marehemu)

Leave a Comment