
MWILI wa mrembo Jemima Oresha aliyetumbukia katika maporomoko ya Thompson Falls Nyahururu nchini Kenya, umeopolewa juzi Jumatano, Agosti 5, 2020 na wakazi eneo la Rwathia kando ya mto ambao waliwajulisha polisi ambao walifika na kuuchukua.
Naibu kamishna wa eneo hilo, Patrick Muli, amesema mwili huo ulipatikana kilomita chache mbali na eneo alikotumbukia na kwamba Jemima (39) alikuwa ametembelea Thompson Falls kufurahia mandhari ya eneo hilo ambapo alikuwa amesimama kwenye jiwe huku ndugu yake, Mangafu, akimpiga picha kabla ya kukumbwa na umauti uliotokana na kutumbukia katika maji ya maporomoko hayo.
Kikosi kilichowashirikisha maofisa wa KWS, polisi, kitengo cha dharura na wale wa Msalaba Mwekundu kilipiga kambi katika mto huo kuusaka mwili wa marehemu.
“Mwili huo ulionwa na wakazi eneo la Rwathia kando ya mto ambao waliwajulisha polisi waliofika na kuuchukua,” Muli alisema.

Naibu kamishna huyo aliwatahadharisha wakazi na kuwaomba kuwa waangalifu wakati wanavuka mito iliyofurika eneo hilo.
Jmima alikuwa amesafiri kutoka Kitale kaunti ya Trans Nzoia na alisisitiza kwamba kabla ya kurejea nyumbani angependa kuzuru maeneo hayo yenye mandhari ya kupendeza.