SERIKALI ya imesema kanuni mpya zinazoongoza huduma za maudhui ya mtandaoni na zile za radio na televisheni hazijaanza leo, ni kanuni zilioanza kufanyiwa mchakato zamani na zimeshirikisha wadau wote waliopo kwenye tasnia hizo kwa kushirikiana na Serikali yenyewe.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Agosti 11, 2020, na Dkt. Hassan Abbas, Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akifanyiwa mahojiano na Front Page ya +255 Global Radio.
“Kuna wanaosema kanuni mpya zinatekelezwa na TCRA lakini zimesainiwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, kumbuka kwamba hizi kanuni ni za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambayo kwa mujibu wa sera ya taifa, TCRA inawajibika kwenye Wizara mbili, yaani Wizara ya Habari na ile ya Uchukuzi na Mawasiliano.
“Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 pia imefafanua hilo, Sheria inatungwa lakini kanuni zinatungwa na Mamlaka inayotekeleza sheria hiyo. Wizara ya wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, hii inasimia mambo ya habari, wasanii, na wanamichezo.
“Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano inasimamia teknolojia za mawasiliano, watoa huduma za mawasiliano, uchukuaji wa masafa na kuyasafirisha, mitambo, minara na vitu vingine kama hivyo, zingekuwa kanuni zinazosimamia mitambo ya mawasiliano zingesainiwa na Waziri wa Mawasiliano, lakini kwa sababu zinasimamia maudhui ya habari ndiyo maana zimesainiwa na Waziri wa Habari.
“Wanaosema hazijahusisha wadau siyo sahihi, kanuni mpya za maudhui ya mitandaoni mchakato wake umeanza zamani, wakati naingia kwenye ukatibu mkuu, zimeshirikisha wadau na wametoa maoni yao kwa mara ya kwanza, baadaye tena tukawarudishia kwa mara ya pili tena tukawaelekeza walete kwa maandishi.
“Watu wanasema kanuni hizi zimekuja wakati wa uchaguzi, tuachane na uchaguzi, nchi ipo kabla na baada ya uchaguzi, wewe ulitaka tufanye lini? Zile kanuni zimekuja kulingana na uzoefu ambao tumeupata kwenye miaka hii minne, kila nchi sasa inaunda sheria na kanuni kudhibiti mambo holela kwenye mitandao, uhuru binafsi kuingiliwa, taarifa za uongo, chochezi na hatarishi,” amesema.
