×

Tonombe, Tuisila Watua Dar Kibabe

WACHEZAJI wapya wa Yanga, winga Tuisila Kisinda na kiungo mkabaji, Mukoko Tonombe wanatarajiwa kutua kibabe jijini Dar leo Alhamisi baada ya kupata vipimo vya Covid-19.

 

Hiyo ni baada ya Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga na Mkurugenzi Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Injinia Hersi Said kukamilisha dili la usajili wa nyota hao.

 

Ujio wa wachezaji hao kutaimarisha safu ya ushambuliaji na kiungo baada ya kuwatema wachezaji 16 wakiwemo wakongwe Kelvin Yondani, Juma Abdul na Papy Tshishimbi.

 

Kwa mujibu wa Hersi, wachezaji hao walitarajiwa kutua nchini juzi, lakini ilishindikana kutokana na kusubiria vipimo vya Covid-19 vitakavyowaruhusu kutoka nchini kwao DR Congo.

 

Jana Jumatano baada ya majibu ya vipimo hivyo kutoka, walianza safari ya kutoka DR Congo kupitia Ethiopia na kutua Tanzania tayari kuungana na wenzao katika mazoezi ya pamoja.

 

“Ninatarajia kutua nchini Alhamisi (leo) na wachezaji wetu wapya Tonombe na Tuisila tukitokea DR Congo, tayari kwa kuungana na wachezaji wenzao mazoezini.

 

“Kikubwa kilichotuchelewesha kutua Tanzania ni vipimo vya Covid-19 kutoka kwa wachezaji hao, kwani nchi yao huwezi kutoka bila ya kupima kipimo hicho,” alisema Hersi.

 

Mashabiki wa Yanga leo Alhamisi wamepanga kuwapokea nyota wao hao wapya ambao wakitua tu, moja kwa moja wanakwenda kambini kuanza maandalizi ya msimu wa 2020/21.

WAGOMBEA UBUNGE CCM KUCHEKA, KULIA LEO | RUNGWE AFUNGUKA SERA YA UBWABWA KUINUA ELIMU

Leave a Comment