KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi, Comrade Amir Mkalipa amesema chama hicho hakijatetereka na kuondoka kwa aliyekuwa kada wake wa muda mrefu na kiongozi wa chama hicho, Bernard Membe, ambaye hivi karibuni ametimkia ACT Wazalendo na kupitishwa kuwania urais kupitia chama hicho.
Mkalipa amesema hayo leo Jumatatu, Agosti 24, 2020 wakati akifanya mahojiano na Kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio.Â
“Mkoa wa Lindi hakukuwa na malalamiko yoyote kuhusu uteuzi wa wagombea, wajumbe kazi yao ilikuwa maoni na wagombea tuliwaeleza, kwa kweli sisi tumevuka salama, maoni ya wajumbe na maamuzi ya vikao yamezingatiwa.
“Hili jina limeibuka na kupata umaarufu sana, lakini wajumbe wa CCM ni watu makini sana, ukitaka uthibitishe umakini wao angalia namna walivyowavusha wagombea na namna walivyowakataa watia nia, ukiwa na dharau sana utakataliwa.
“Ili uwe mjumbe lazima uwe kiongozi, hawa ndiyo mashine zetu pale kwenye tawi na ndiyo wanaendesha shughuli za chama, kuna wajumbe wa aina tofauti, tawi, kata mpaka Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wapo kila siku na kazi yao ni muhimu ndani ya chama.
“”Sisi wenezi ndiyo wasemaji wa chama, tunatekeleza Ilani ya CCM, tukikuta sehemu Ilani yetu haijatekeezwa ipasavyo lazima tuwe wakali. Mfumo wa CCM unaandaa sana vijana, uongozi ni generation (kizazi), vijana wa CCM tupo timu B, tunachukua mmoja mmoja tunampeleka timu A, na Mheshimiwa Rais ametuamini, ameteua vijana wengi sana kwenye chama na serikali.
“Membe mnamkuza sana, kwetu Lindi sidhani kama ana sifa za kuwa rais, sisi Wana-Lindi tunamjua vizuri. Bernard; amekuwa mbunge kwa miaka 15 na waziri, lazima angefanya makubwa. Hata kijijini kwakwe Rondo umeme umeletwa na Rais Magufuli.
“Lindi imeunganishwa kwenye gridi ya taifa, tutakuwa si wenye busara kumchagua mtu kisa katoka kwetu, sisi hatutafuti rais kwa sababu anatoka mkoani kwetu, tunatafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kata ya Rondo-Chiponda ambapo Membe ndipo amezaliwa, tumefanya uchaguzi wa madiwani, wajumbe wote kuanzia mashina wameshiriki na wapo CCM. Mzee Lowassa alipoondoka alikwenda na viongozi wa chama wa mikoa, lakini leo tupo.
“CCM ni taasisi kubwa Afrika na duniani, tafiti zimefanywa ndani ya chama chetu na zinaonyesha kura za urais Lindi tutapata zaidi ya asilimia 90…” amesema Mkalipa.
