TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema imepokea mapingamizi kutoka kwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipasi Lissu, dhidi ya wagombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli na Prof. Ibrahim Lipumba kupitia Chama cha Wananchi (CUF).
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Wilson Mahera, amesema kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi masharti ya kanuni ya 39(5) ya Kanuni za Uchaguzi za Rais na Wabunge za Mwaka 2020, baada ya kupokea mapingamizi dhidi ya wagombea hao, imewaarifu wawekewa mapingamizi mapema ili waweze kuwasilisha utetezi wao.
Kuhusu pingamizi kuwa Lipumba hakurejesha fomu za uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa kisheria, NEC imesema baada ya kupitia pingamizi na utetezi imejiridhisha kuwa Lipumba amerejesha fomu kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelezo ya tume.
Kuhusu mapingamizi dhidi ya Magufuli kuwa hakuambatanisha picha kwenye fomu ya uteuzi na kuwa hakurudisha fomu ya uteuzi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria, tume imesema imepitia mapingamizi yote na utetezi uliotolewa na kujiridhisha mapingamizi hayo hayana msingi kwani Magufuli alirejesha fomu zenye picha na kwa mujibu wa sheria na kanuni.
