
MGOMBEA Ubunge wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Vunjo Dkt .Charles Kimei jana Jumamosi amewaomba wananchi wa Jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuwa Mbunge wao ili aweze kuwaletea mapinduzi ya kiuchumi.
Aliyasema hayo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika katika Mji mdogo wa Himo na kuratibiwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Jimbo hilo.
Katika hotuba yake, Dkt.Kimei alisema kuwa Jimbo hilo lina changamoto nyingi ikiwemo miundombinu mibovu ya barabara, Elimu, Afya na ukosefu wa masoko thabiti kwa mazao yazalishwayo na wakazi wa jimbo hilo.
Alisema kuwa, ikiwa wananchi watamchagua kuongoza jimbo hilo, atatumia uzoefu wake katika sekta ya fedha kuanzisha Mfuko wa Ujasiriamali wa Jimbo ambao utahusika kutoa mikopo nafuu kwa wanachi ili kuwapa uwezo wa kujiajiri na kuajiri ili kuwapaisha kiuchumi.
Kwa kushirikiana na wadau wengine, tunakamilisha mchakato wa kuanzisha mfuko wa Wajasiliamari Vunjo.

Mimi mwenyewe nitatoa andiko la mradi yaani (Project write-up) ili kupata fedha za uwezeshaji wa makundi maalum ya Wakulima, Wafugaji, Vijana, Wanawake, Waendesha Bodaboda na Mafundi Makenika kwa kuwapa mikopo nafuu”.
Kuhusu Kilimo na mazao ya shambani, Dkt. Kimei alizungumzia kuhusu kuanzishwa Kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija, sambamba na kuwawezesha wananchi kuanzisha viwanda vya usindikaji hivyo kuongeza thamani ya mazao.
Jambo kubwa la msingi ni kuanzisha viwanda vya usindikaji ili kuongeza thamani ya mazao yetu.
Badala ya kuuza mpunga, tutaanza kuuza mchele wetu uliofungwa vizuri. Badala ya kuuza nyanya ambazo uharibika kirahisi, viwanda hivi vitasindika nyanya hizo na tutauza tomato paste yetu wenyewe hivyo kuongeza thamani na vipato vya wananchi wa Himo.
Tutafanya hivyo pia kwa mazao ya Kahawa na mengineyo’ alisema Dkt.Kimei.
Aliongeza kuwa, eneo lingine ni kuboresha miundombinu ya Barabara ili kurahisisha usafarishaji wa mazao hayo ili kufikia masoko kwa urahisi kutokana na hali hiyo, maisha ya wananchi yatabadilika na kupiga hatua za kimaendeleo.

Kwa upande wa changamoto Dkt.Kimei alisema kuwa vituo vingi vya afya vinahitaji ukarabati mkubwa wa haraka huku vikikosa vifaa vya kisasa kama X-RAY na Ultra-sound;
“Tutasimamia kukamilisha ujenzi wa hospitali wa wilaya ya Himo ambao ulisimama. Pia tutashughulikia masuala ya Bima za afya na matibabu kwa Wazee. Kuhusu ukosefu wa gari la Wagonjwa, Dkt. Kimei alisema;
“Kwa sasa, jimbo letu halina gari la uhakika la kubebea wagonjwa hivyo naahidi kutoa gari langu mimi mwenyewe, lifanye kazi hiyo wakati tunaendelea na mchakato wa kuongeza mengine” alisema.
“Nimejipanga kuhakikisha wananchi wa Himo wanapata maendeleo kama inavyosema ilani ya Chama cha Mapinduizi.
“Nitashirikiana na Serikali kila nyanja ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kunufaika na rasilimali zao.” Alisema Dkt. Kimei.
Aidha, pia mbali ya kujiombea kura, pia aliweza kumuombea kura nyingi na za kishindo kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Madiwani wote ndani ya jimbo hilo la Vunjo.