×

Wasafi Watoa Tamko Kufuatia Tuhuma za Kutumia Nguvu za Giza!

KWA muda mrefu sasa, kumekuwa na madai mazito kwamba, mwanamuziki mkubwa nchini Tanzania, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na wenzake walio chini ya lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), wanatumia uchawi ili muziki wao ukubalike ndani na nje ya Bongo.

 

Mbali na Diamond au Mondi, memba wengine wenye skendo hiyo ndani ya Wasafi, ni Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’, Abdul Iddi ‘Lava Lava’, Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ na Zuhura Othman ‘Zuchu’ ambao wanadaiwa kuishi maisha ya kitajiri kwenye majumba ya kifahari na kuendesha magari ya bei mbaya, baada ya kutusua kwenye muziki kwa kutumia nguvu za giza.

 

Mbali na kutumia nguvu za giza, pia memba hao wanadaiwa kujiunga na jamii za siri za kishetani (kama Secret Society, Freemason, Illuminate na nyinginezo) ambazo hujishughulisha na kutoa makafara ya damu na uhai wa watu ili kujipatia utajiri mkubwa kwa haraka.

TAMKO ZITO

Kufuatia tuhuma hizo za matumizi ya nguvu za giza kuendelea kushika kasi kila kukicha, uongozi wa Wasafi umelazimika kutoa tamko zito juu ya jambo hilo.Skendo ya wasanii kutumia ushirikina, imekuwa ikisikika kwenye vyombo vya habari, ambapo baadhi yao wamekuwa wakilizungumzia suala hilo la uchawi, wakikiri kwamba lipo sana kwenye sanaa ya muziki nchini.

 

MKUBWA FELLA…

Uongozi wa Wasafi kupitia kwa mmoja wa mameneja wake, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ umetoa tamko la kukemea skendo hiyo inayohusishwa na wanamuziki wa lebo hiyo kubwa ya muziki barani Afrika.Tamko hilo linakuja wiki moja tangu Diamond au Mondi kudaiwa kunaswa na hiziri kiunoni alipokuwa akipafomu kwenye shoo kubwa ya uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mkubwa Fella.

Tuhuma hizo zimekuwa zikishadadiwa na mwanamuziki wa kitambo nchini Tanzania, Hamis Baba ‘H. Baba’ ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitangaza kuwa, Mondi na wasanii wake wanatumia uchawi kupaisha muziki wao.

 

Fella ameliambia Gazeti la Risasi Jumamosi;“Kwanza hili ni tamko rasmi na nisingependa kutaja majina ya watu wanaoeneza hilo jambo ili kumchafua au kuwachafua wanamuziki wa Wasafi.“Tuhuma hizi siyo mpya hata kidogo, tumezisikia kwa miaka mingi huko nyuma.

 

“Unajua mti wenye matunda ndiyo unapigwa mawe, watu watakushangaa wakikuona unarusha mawe kwenye mti ambao hauna matunda. Diamond ni mti wenye matunda. Tunaona mambo mengi mitandaoni, lakini huwa haitusumbui kwa sababu hao ni watu wenye lengo la kuchafua brand yetu na wasanii wetu.”

WASAFI NI KUBWA

“Kama kuna mtu hajui, wakati Diamond anaanzisha Wasafi. Neno Wasafi lilikuwa likisikika kwenye nyimbo zake nyingi, lakini wengi walidhani zilikuwa mbwembe tu.“Diamond alikuwa anajua anapoelekea na Wasafi hakuitaja tu bure, alijiona hapa alipo sasa.

 

“Hakuna aliyetegemea Wasafi itakuja kuwa lebo kubwa ya kusamimia wasanii na kufanya biashara mbalimbali za muziki, lakini ndilo tunaishi nalo kwa sasa.“Maneno kama hayo ya kutumia nguvu za giza kwenye muziki au kwenda kwa waganga, hizo ni kelele tu za wapinzani wake, lakini hakuna kitu kama hicho.

 

MONDI ANAWEKEZA…

“Najua watu wengi wanaoongea mambo hayo, kuna kitu hawakijui, lakini siri ni moja tu, Nasibu (Mondi) ni mwanamuziki mkubwa aliyewekeza sana kwenye muziki wake. Tunapozungumzia uwekezaji si pesa pekee, bali hata muda na nguvu kubwa katika kufanya shoo kubwa.

 

“Unajua kuna wasanii wana uwezo mkubwa sana, lakini wamekuwa wagumu kuwekeza, mikono yao imekuwa migumu kuzama mfukoni na muda wao mwingi umekuwa ukichukuliwa na mambo yasiyokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na muziki wao. “Nasibu (Mondi) anafanya kitu anachokipenda, anapenda muziki wake ndiyo maana anaweka pesa nyingi kuwekeza kwenye muziki.

 

HAKUNA UCHAWI

“Kwa kufanya hivyo, Nasibu (Mondi) anajihakikishia kuendelea kutawala Bongo Fleva kwa kipindi kirefu zaidi, wala hakuna uchawi hapo,” alimalizia Fella ambaye leo (Jumamosi) anazindua kampeni zake za Udiwani wa Kata ya Kilungule wilayani Temeke jijini Dar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

 

TUJIKUMBUSHE

Kufuatia tuhuma hizo, Mondi mwenyewe amekuwa akisema; “Ndiyo mimi ni mchawi na uchawi wangu ni ubunifu wangu, lakini mti wenye matunda, ndiyo hupigwa mawe.“Kumchukia Diamond na kutegemea unaweza kumshusha, ni kujipa maumivu.”

STORI: MEMORISE RICHARD, RISASI JUMAMOSI

Leave a Comment