
Baada ya Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) kutoa mafunzo ya kutengeneza nishati mbadala katika vikundi mbalimbali, kikundi cha Sauti ya Jamii kimerejesha kile ambacho wamejifunza ambapo tukio hilo limefanyika mapema leo maeneo ya Kipunguni jijini Dar.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo Mkurugenzi wa kikundi cha Sauti ya Jamii kilichopo Kipunguni Dar, Selemani Bishagazi amesema kuwa takataka zinazozalishwa mitaani zinaweza zikatumika na kutengeneza vitu vingine na kuendelea kutumika kwa matumizi mengine.
“Tulipata mafunzo ya kutengeneza nishati mbadala kutoka Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) ambayo yalikuwa ya siku tatu baada ya hapo tumekuja kurejesha kwa jamii kile ambacho tumejifunza.
“Baada ya kuona mitaani takataka zinasambaa ovyo na kwenye mitaa mingine watu wanalipa wakandarasi kwa ajili ya takataka sisi tukaona tuzikusanye tuweze kutengeneza vitu vingine kwa matumizi mengine.

“Tumechukua makabiki ya maboksi yaliyotupwa kama uchafu na kutengeneza mkaa ambao utatumika kwa matumizi ya jikoni, makaratasi tumetengeneza mapambo ya ndani na vikapu ambavyo unaweza ukahifadhia vitu mbalimbali.
“Na pia kuna sehemu hizi ambazo wanauza mkaa yale mabaki ya mkaa wanayatupa kwa hiyo sisi tunayachukua na kuyatwanga na kuchanganya na unga wa muhongo ambapo tunazalisha mkaa mwingine ambao utatumika tena na ni bora zaidi kuliko mkaa wa mwanzo.
“Tunaona magogo yanakatwa kwa ajili ya kutengeneza mkaa kumbe tungeweza kutengeneza mkaa kwa kutumia chenga na vumbi lake kuzalisha mkaa mwingine.

Kwa hivyo tunaomba Serikali iwekeze kwenye hivi vitu vya nishati mbadala tunaweza tukaisaidia kuepuka matumizi mengine ambayo ni ya ziada.
Nae mwanakikundi, Frevia John amesema kuwa wamejifunza kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo vinawasaidia kupata kipato.
“Tumejifunza kutengeneza mapambo kutokana na uchafu wa makaratasi, pia tumejifunza kutengeneza mkaa ambao tunauuza sisi kama kikundi na tunapata fedha tunagawana na kuendesha maisha yetu kwa sababu siyo kila kitu ukawe tegemezi kwa mwanaume.” Alisema Frevia.