SAA kadhaa baada ya mwanamitindo wa kimataifa wa Tanzania, Hamisa Mobeto ‘Misa’ kuposti video mtandaoni akiwa na mzazi mwenzake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mtoto wao, Abdul Nasibu ‘Dyllan’, hali imekuwa si shwari.
Habari zilizolifikia Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, zimedai kuwa, ishu hiyo imeufanya ushosti wa Mobeto na mzazi mwingine wa Diamond au Mondi, Tanasha Donna kuwa shakani.
Hivi karibuni, Mobeto na Tanasha walitangaza ushosti wao rasmi na kwamba wapo tayari kuwaunganisha watoto wao; Dyllan na Naseeb Junior, kwa sababu ni damu moja; yaani wote wamezaa na Mondi.
Wawili hao walikwenda mbali zaidi na kusifiana kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii na kuganga yajayo, kwani yaliyopita si ndwele. Pia, kama hiyo haitoshi, kwenye wimbo wa Tanasha wa Liar, Mobeto ndiye aliyesimamia shughuli nzima ya upambaji na mavazi katika kung’arisha video ya wimbo huo.
Inadaiwa kwamba, video aliyoiposti Mobeto, haikumfurahisha Tanasha ambaye amekuwa akilalamika kutelekezewa mtoto na Mondi, hivyo kujikuta akimlea mwanaye Naseeb Junior bila msaada wa jamaa huyo. Inaelezwa kuwa, baada ya kuona amemkwaza shoga’ke huyo, Mobeto alimtumia Tanasha ujumbe wa msamaha ambapo mwanamama huyo alimjibu kwa kifupi; “It’s okey baby…”
Gazeti hili la IJUMAA WIKIENDA, lilimtafuta Mobeto ambaye alifunguka kuwa, yeye na Tanasha hawana tatizo lolote na kwamba wanasapotiana kama kawaida na kupuuza habari zinazosambaa mitandaoni kuwa wametibuana kwa sababu ya Mondi.
“Hakuna tatizo kati yetu, tunasapotiana kama kawaida, tuyapuuze mambo ya mitandaoni,” alisema Mobeto kwa kifupi.
Akizungumzia urafiki wake na Mobeto, hivi karibu Tanasha alikaririwa akisema; “Hamisa (Mobeto) amekuwa ni mtu ambaye ninakubali kazi zake, maana ni mchapakazi na ana upendo. Hivyo, nimepanga kuwakutanisha watoto wetu, maana wao ni ndugu wa baba mmoja. “Na watoto wetu wamekuwa wakizungumza kwenye video call mara nyingi tu.”
STORI: IMELDA MTEMA, DAR
