
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Buchosa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo, amewaomba wanachama wa chama hicho na wananchi wote wa jimbo hilo kujitokeza kuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Kauli hiyo ameitoa jana Septemba 23, 2020 kwenye mkutano wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Makoye Agustine, wakati alipokutana na mabalozi, wenyeviti na madiwani ambao hawakupata nafasi ya kuteuliwa katika nafasi za udiwani kwenye mchakato wa kura za maoni.

Katika mkutano huo Shigongo amewaomba kuachana na yaliyopita kwenye mchakato wa kura za maoni na badala yake wanachama wa CCM wajikite katika kutafuta kura za ushindi katika uchaguzi ujao.
“Nawaombeni muondoe tofauti zenu kwani uchaguzi ndani ya chama chetu ulikwisha hivyo tuunganishe nguvu zetu katika kukipigania chama ili kiweze kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020,” alisema Shigongo.

Aidha, Shigongo amewataka wanachama na wanachi kujitokeza kawenye uzinduzi rasmi wa kampeni zake utakaofanyika kesho Ijumaa, Septemba 25,2020 katika uwanja wa Kijiji cha Nyakaliro.

Uzinduzi huo utafanywa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 12 jioni.
Aidha, uzinduzi huo utasindikizwa na wasanii kibao watakaotumbuiza wakiwemo Young Killer, H-Haba, Paul Clement, Joel Lwaga, Jane Misso, Ronna Max, Dox Flavour na wengine kibao kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza.
