×

Polepole Awalipua Chadema, ACT “Ni ‘Majambazi’ wa Kisiasa” – Video

KATIBU wa Idara ya Itikadi na Uweneziwa Chama cha Mapinduzi CCM, Humphery Polepole amesema kwamba chama cha Mapinduzi CCM kimetoa maelekezo kwa wagombea wake wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na visiwani Zanzibar kujikita zaidi katika kunadi sera pamoja na muelekeo wa nchi endapo watachaguliwa na wananchi.

 

Polepole amesema kuwa CCM kwa sasa wanajikita zaidi katika kuwaonesha watanzania wapi nchi inapoelekea ila wapinzani wao wanadi sera za uongo pamoja na kujikita katika kupotosha Watanzania.

 

Hayo amayaeleza leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalumu uliofanyika ofisi kuu za Chama cha Mapinduzi CCM, Zanzibar, Kisiwandui Mjini Unguja.

 

Polepole alisema, Chama cha Mapinduzi CCM kwa hiari yake imeamua kutoa maagizo wa wagombea wao kujikita zaidi kutangaza muelekeo wa nchi wanapotaka kuifikisha.

 

“Tumewaambia watangaze sera na muelekeo wa Taifa tunapotaka kulifikisha na si kutangaza tulichokifanya hapo nyuma maana watanzania tayari wameshayaona maendeleo makubwa yaliyofanywa na Chama cha Mapinduzi CCM,” alisema Polepole.

 

Aliongeza kusema kwamba Wagombea wote ambao ni Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Dk. Hussein Ali Mwinyi wajikite katika kutangaza maono ya nchi wanapotaka kuifikisha pamoja na kutangaza maono yalikuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020/2030.

 

“Mbali na kutangaza maono yao, wajikite zaidi katika kutangaza muelekeo wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM 2020/2030 huko kuna kila kitu ambacho kinaonesha wapi ambapo CCM inataka kuifanyia nchi hii,” alisema Polepole.

“Dkt. Mwinyi unaweza kumlinganisha na huyu Babu yenu? Alishaondoka zake CCM sisi hatumhitaji, alikwama hapa akapewa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Juzi alipokwenda kuchukua fomu wafuasi wake wanasema piga, ua na yeye anasikia tu bila kuwakemea.
“Juzi Pemba wanachama wa chama chake, mtu anakwenda Msikitini wakati wa Ibada anapiga panga watu, miaka ya nyuma mashehe walimwagiwa tindikali, mapadre wakauawa, hakuna aliyekamatwa, msilete mambo ya kibwege, hii ni zama za Amri Jeshi Mkuu Magufuli.
“Tangu mwaka 1995 Zanzibar anaegombea ni babu madevu ,2020 babu madevu hata 2025 Mgombea atakuwa huyo huyo babu madevu, ina maana humo kwenye taasisi hakuna Vijana wenye fikra za uongozi? Babu madevu mimi najua shida yake amekuwa na desturi ya kutajataja watu, sasa mimi nimeshakuja Zanzibar, tunataka watoto wadogo babu madevu wamfundishe adabu,” amesema Polepole.

Alifafanua kuwa tayari Dk. Magufuli na Dk. Mwinyi pamoja na viongozi wengine kama vile Kassimu majaliwa pamoja na Samia suluhu Hassani wameshapita kutangaza muelekeo wa chama hicho.

 

Katika hatua nyingine Polepole alisema kwamba chama cha Mapinduzi CCM kinaendelea na kampeni zake kama ratiba zilivyopangwa ambapo hadi sasa tayari makundi mbalimbali tumeshafikia kwa lengo la kunadi sera zao.

 

“Kwa upande wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wagombea wetu wameshawafikia makundi hayo na wanaendelea na Kampeni zao”alisema Polepole.

 

Leave a Comment