×

Mpakstani Anaswa Akidaiwa Kuingia TZ Kinyemela

IDARA ya uhamiaji mkoani Kagera inamshikilia  raia wa Pakstan, Mohammed Adinani Tahir, anayedaiwa kuingia nchini kinyume na taratibu akitokea nchini Uganda baada ya Rais  John  Magufuli kutangaza Tanzania ni salama na hakuna Corona.

 

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mjini Bukoba Oktoba 8,mwaka huu, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera Kamishina Msaidizi, Hamza Ismail Shaban, amesema mtuhumiwa alikamatwa Oktoba 7, 2020,  uwanja wa ndege wa Bukoba  akitaka kupanda ndege kuelekea jijini Dar es Salaam.

 

Alisema mtuhumiwa aliingia Tanzania upande wa Kagera akitokea nchini Uganda kwa kupita njia zisizo rasmi.

Ameongeza kuwa baada ya Rais Magufuli kuitangazia dunia kuwa Tanzania hakuna Corona na shughuli zinaendelea kama kawaida na kuongeza kuwa raia huyo alipata taarifa hizo na kuamua kukimbilia Tanzania na baada ya kuingia akagundua kuwa hakuna Corona ambapo ameeleza kuwa uwepo wake hapa nchini sio rasmi kwakuwa ameingia kinyemela na anaishi nchini kinyume cha sheria.

 

Kamishina Shaban ametumia fursa hiyo kuwataka raia wanaotaka kuingia Tanzania kufata taratibu zilizowekwa na nchi yetu pamoja na kuwataka watanzania wazalendo kuhakikisha wanawabaini watu wanaoingia nchini kinyemela na kuwatolea taarifa mahala popote watakapo waona.

 

“Nitoe rai kwa watanzania wazalendo kuwa wasiwe sababu ya watu ambao sio watanzania au ambao hawana vibali vya kuwa hapa nchini kuingia na kuwahifadhi badala yake watoe taarifa kwa idara ya uhamiaji au kwa viongozi wa serikali mahali walipo, kama tunavyojua nchi yetu tupo kwenye mchakato wa uchaguzi hivyo hatupaswi kuruhusu watu wasiokuwa raia au tusiowajua kuingia hapa pasipokujua lengo lao,” amesisitiza Shaban.

 

Kwaupande wake mtuhumiwa huyo amesema kuwa amekuja Tanzania baada ya kukaa LOCKDOWN nchini Uganda kwa takribani miezi 6 kutokana na janga la Corona na aliposikia Tanzania hakuna Corona alijaribu kutumia njia mbadala za kuweza kumfikisha hapa nchini ambapo ameeleza kuwa alikuja kwa gari ndogo aina ya Tax.

 

Amesema kuwa amekuwa akija Tanzania mara kwa mara kutokana na biashara zake anazozifanya hapo awali kabla ya nchi nyingi kufunga mipaka yake kutokana na Corona hivyo Tanzania anaijua.

Na Allawi Kaboyo- Bukoba.

Leave a Comment