MGOMBEA ubunge Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, ametembelea ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kijiji cha Katoma iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa miaka 10 bila kupata msaada kutoka mfuko wa jimbo ambapo jengo hilo limebaki kuwekewa milango, madirisha pamoja na finishing.
Shigongo amewaahidi wananchi hao kuwa iwapo atachaguliwa, kwa kushirikiana na Serikali basi atahakikisha jengo hilo linakamilika haraka iwezekanavyo ili lianze kutumika na kuokoa maisha ya akina mama na watoto ambao wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu.
Mgombea huyo amesema kuwa suala la kuboresha sekta ya afya katika vijiji vya Buchosa ni la lazima, hivyo atahakikisha anafanya juhudi zote kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati kila kijiji kama Ilani ya CCM inavyoeleza, kupeleka madawa na vifaa tiba ili wananchi wapate huduma iliyo bora.
Aidha, alipata nafasi ya kutembelea kina mama waliojifungua kwenye zahanati hiyo na kuwapongeza pamoja na kuwatia moyo wawe wazazi bora kwa watoto wao kwa kuwatengezea mazingira mazuri yatakayowasaidia kutimiza ndoto za watoto hao.
Shigongo anaendelea na kampeni zake jimboni Buchosa akinadi sera za chama chake cha CCM pamoja na kuwaomba ridhaa wananchi ili wawachague viongozi wa CCM kuanzia kiti cha urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.







