×

Sarpong, Moro out Yanga

IMEFAHAMIKA kuwa Yanga rasmi imeachana na mastaa wake wawili Waghana, Lamine Moro na Michael Sarpong katika kuelekea msimu ujao.

 

Yanga wataachana na wachezaji hao wakiwa wamebakisha mwaka mmoja katika mikataba yao waliyosaini msimu huu kama wachezaji huru.

Mastaa hao hawapo kambini kwa zaidi ya wiki mbili ambapo Kocha Mkuu wa timu hiyo raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi aliwatimua kwa utovu wa nidhamu.

 

Mmoja wa mabosi wa Yanga mwenye ushawishi mkubwa katika usajili, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, mabosi wa timu hiyo wamewaondoa wachezaji hao katika mipango ya msimu ujao.

 

Bosi huyo alisema kuwa, wachezaji hao hawapo kambini kwa kipindi hicho baada ya kocha Nabi kutokuwa katika mipango yake katika michezo waliyoibakisha ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

 

Aliongeza kuwa hivi sasa kamati ya mashindano ya timu hiyo chini ya Mwenyekiti, Dominic Albinus ipo kwenye mipango ya kumsajili beki wa kati wa kigeni atakayekuja kumrithi Moro na straika tishio zaidi ya Sarpong.

 

“Mchezaji aliyesimamishwa na uongozi kwa hivi sasa ni Metacha ambaye kesi yake inatarajiwa kusikilizwa leo (jana) ambaye atakutana na Kamati ya Nidhamu ya Yanga.

 

Lakini hao akina Moro na Sarpong hawapo na timu kambini baada ya kocha Nabi kupendekeza kuwaondoa kambini kutokana kutokuwa katika mipango yake ya michezo tuliyoibakisha ya ligi na FA.

 

“Hiyo ni ishara tosha kuwa kocha hawahitaji tena wachezaji hao katika msimu ujao huku akipendekeza wengine watakaokuja kuchukua nafasi zao,” alisema bosi huyo.Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa alithibitisha hilo kwa kusema kuwa: “Sarpong na Lamine hatujawasimamisha kama ilivyokuwa kwa Metacha.

 

Wachezaji hao hawapo kambini baada ya kocha kuwaondoa katika mipango yake ya michezo yetu ijayo ya ligi na FA,” alisema Mfikirwa.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment