KIMBUNGA kiitwacho Molave kimeua watu 18 na wengine 48 kutofahamika waliko hadi sasa nchini Vietnam ambapo mchakato wa uokoaji unaendelea nchini humo baada ya majanga makubwa yaliyosababishwa na maporomoko ya ardhi.
Mamia ya wanajeshi wenye vifaa vizito wametumwa katika maeneo ya ndani ya jimbo la Quang Nam ambako miili ya wavuvi 12 imeopolewa baharini hii leo na wengine 14 hawajulikani walipo baada ya boti yao kuzama. Kimbunga hicho kinatajwa kuwa ni kibaya kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.
Molave kimepiga katikati ya nchi hiyo ambako tayari kumekuwa kukinyesha mvua kubwa kwa wiki kadhaa zilizosababisha vifo vya watu wapatao 160.
Zaidi ya watu milioni moja wameathiriwa na dhoruba hizo kwa wiki kadhaa. Mashirika ya kutoa misaada nayo yameelemewa kutokana na idadi kubwa ya watu walioathirika.
