WINGA matata wa UD Songo ya nchini Msumbiji, Pachoio Lau Ha King ‘Lau King’ amekubali kusaini mkataba wa kukipiga Simba kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu.
Nyota huyo ni kati ya wachezaji wanaotajwa kuwa kwenye mipango ya kusajiliwa na Simba katika usajili wa dirisha dogo litakalofunguliwa mapema Novemba, mwaka huu.
Simba ipo kwenye mipango ya kuiboresha safu ya ushambuliaji katika usajili wa dirisha dogo baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck kupendekeza winga wa kimataifa atakayekuja kuchukua nafasi ya Francis Kahata raia wa Kenya.
Akizungumza na Championi Jumamosi,King ambaye ana miaka 25, alisema kuwa yupo tayari kujiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo kama watampa ofa nzuri ya dau la usajili ambalo yeye atalihitaji.
King alisema kuwa mkataba wake unatarajiwa kumalizika Desemba, mwaka huu, hivyo ametoa nafasi kwa Simba kumfuata kwa ajili ya kufanya mazungumzo.
Aliongeza kuwa anaifahamu vizuri Simba kutokana na kuifuatilia kwa karibu huku akiamini kama akitua Msimbazi, basi ataipambania timu hiyo iweze kupata mafanikio zaidi kwenye michuano ambayo inashiriki.
“Sijazungumza na Simba lakini nipo tayari kutua Simba kwani pia ninaifahamu na ninamfahamu Luis (Miquissone) hivyo walete tu dau lao la usajili kisha tujadiliane.
“Hivi sasa ninaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayonihitaji kwani mkataba wangu unamalizika mapema mwezi Desemba, mwaka huu mkataba haunizuii Simba kunifuata kuzungumza na mimi,” alisema King.
