TIMU ya Masoko ya Global Publishers leo imetua katika Uwanja wa Mkapa na kuyanadi magazeti ya michezo ya Kampuni hiyo ambayo ni Championi na Spoti Xtra leo Ijumaa, Novemba 7, 2020.
Katika Uwanja huo wa Mkapa ambapo leo kuna mechi kubwa ambayo ni Dabi ya Kariakoo kati ya watani wa jadi Yanga SC na Simba SC, timu ya masoko imewapa zawadi ya kuponi ya kuingia kutazama mechi hiyo wasomaji waliokutwa wamenunua na wakisoma gazeti la Championi Ijumaa ili wakaburudike na mechi hiyo ya kihistoria.
Hii imekuwa kawaida ya Kampuni ya Global Publishers kurudisha fadhila kwa wasomaji wake ikiwa ni pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali zikiwemo simu, tisheti, vyombo, gari mpaka nyumba kwenye ikampeni zake mbalimbali.
“Hii imekuwa desturi kurudisha fadhila kwa wasomaji wetu kwani wamekuwa wakituunga mkono sana, hivyo ni jambo jema kuwarudishie kile tunachokipata kutoka kwao, ili na wao wajisikie kama familia ya Championi na Spoti Xtra,” alisema Anthony Adam ambaye ni Mkuu wa Idara ya Usambazaji wa Global Publishers wakati wakigawa tiketi hizo kwa mashabiki.
Mbali na kugawa tiketi za dabi ya Kariakoo, timu ya masoko pia imegawa vipeperushi vinavyolinadi gazeti jipya la Spoti Xtra litakaloanza kutoka hivi karibuni kila Jumanne.
“Tumeamua kutumia hii mechi ya Simba na Yanga kutangaza ujio wa Gazeti letu jipya la Spoti Xtra kila Jumanne ambalo litaanza kutoka hivi karibuni. Gazeti hili litakuwa la kipekee na haijawahi kutokea nchini.
“Nachoweza kuwaambia mashabiki na wasomaji wetu, wakae mkao wa kula, gazeti jipya, bora, lenye mvuto na madini ya kutosha linatua mtaani soon, haya ni maombi ya wasomaji wetu wengi, na sisi tumeamua kuyazingatia, Jumanne, Novemba 17, 2020, litakuwa mtaani rasmi,” alisema Anthony.











