LEO JUMAMOSI ya Novemba 7, itakuwa patashika nguo kuchanika kufuatia miamba miwili ya soka hapa nchini Simba na Yanga kukutana katika Dimba la Mkapa kusaka pointi tatu muhimu.
Timu hizi mara nyingi zinapokutana huwa na upinzani wa hali ya juu kutokana na kila upande kuhitaji kuibuka na pointi tatu muhimu ambazo zitatoa mwanga kuelekea katika kutwaa ubingwa wa ligi mwisho wa msimu.
Novemba 7, Simba na Yanga zitakutana kwa mara ya nne katika mwaka huu wa 2020, ambapo mchezo wa awali walicheza Januari 4 matokeo yalikuwa 2-2.
Mchezo wa pili walikutana Machi 8, Yanga iliibuka na ushindi kwa bao 1-0, lililofungwa na Bernard Morrison na mchezo wa tatu walikutana katika mechi ya Kombe la FA, Simba iliibuka na ushindi mnono kwa kufunga mabao 4-1, hivyo mchezo huo unatarajia kuwa na upinzani wa hali ya juu ambapo kila upande utahitaji kulipa kisasi kwa mwenzake.
Championi Ijumaa linakuchambulia nyota ambao walikuwepo katika dabi iliyopita na sasa watakosekana.
KELVIN YONDANI
Ni mingoni mwa mabeki bora ambao waliwahi kutokea ndani ya Yanga na ni miongoni mwa mchezaji ambaye aliwahi kucheza dabi nyingi za Simba na Yanga hapa Bongo.
Yondani ambaye ameachana na Yanga katika msimu huu alianzia kucheza dabi alipokuwa Simba ambayo ilimsajili mwaka 2008 na kutimka katika kikosi hicho mwaka 2013 na kutua Yanga ambayo ameachana nayo msimu huu wa 2020/21. Kwa mara ya kwanza hatakuwepo katika dabi hii baada ya zaidi ya misimu 10 aliyocheza katika timu hizo kongwe.
JUMA ABDUL
Alikuwa beki wa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea timu ya Indeni FC ya Zambia ambapo ametua huko baada ya kuachana na Yanga.
Juma naye hatakuwepo katika dabi hii ya Novemba 7, lakini dabi iliyopita ya FA alikuwa miongoni mwa kikosi cha Yanga.
MRISHO NGASSA
Alikuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga ambaye amewahi kuichezea timu hiyo kwa vipindi tofauti tofauti na ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kucheza dabi nyingi za Simba na Yanga.
Safari hii hatakuwepo katika mchezo huu licha ya dabi iliyopita alikuwa sehemu ya wachezaji walioivaa Simba. Kwa sasa anakipiga Ndanda FC ya Mtwara inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
YIKPE GISLEIN
Mshambuliaji raia wa Ghana alitua Yanga msimu uliopita lakini hakuweza kudumu na badala yake aliachwa kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika kikosi hicho, hivyo hatokuwa sehemu ya kikosi cha Novemba 7.
DAVID MOLINGA
Mshambuliaji aliyewahi kuichezea Yanga msimu uliopita na kuipambania kwa hali na mali, pia alikuwepo kwenye dabi iliyopita lakini hii ya Novemba 7 hatakuwepo kutokana na kuachwa katika kikosi hicho.
ANDREW VICENT ‘DANTE’
Beki wa kati aliyeichezea Yanga msimu uliopita, lakini msimu huu si miongoni mwa wachezaji wa Yanga kuelekea dabi ya Simba na Yanga Novemba 7. Msimu uliopita hakupata nafasi mara nyingi kutokana na mgogoro wa kimaslahi kati yake na uongozi wake.
SHIZA KICHUYA
Aliichezea Simba msimu uliopita, alikuwa miongoni mwa kikosi kilichoivaa Yanga katika mzunguko wa pili kwenye Kombe la FA. Lakini katika mchezo huu hatakuwemo kwani sasa anakipiga Namungo.
SHARAF SHIBOUB
Kiungo huyu Msudan alisajiliwa na Simba msimu uliopita lakini hakucheza hata mechi moja ya dabi na mwisho wa msimu akapigwa chini.
DEO KANDA
Kiungo huyu mshambuliaji alipata nafasi ya kuicheza Simba katika mchezo wa dabi za msimu uliopita lakini msimu huu hatokuwepo kutokana kwani aliachwa kikosini hapo.
TAIRONE SANTOS
Mbrazil aliyeichezea Simba msimu uliopita, alikuwa sehemu ya kikosi kilichocheza dabi ya Simba na Yanga lakini Novemba 7 hatakuwa sehemu ya kikosi kutokana na kuachwa na timu.
WENGINE WA SIMBA: Yusuph Mlipili, Haruna Shamte na Rashid Juma.
WENGINE YANGA: Raphael Daud, Ally Ally na Ally Mtoni ‘Sonso’.
Makala- Bongo | KHADIJA MNGWAI | DAR ES SALAAM
