SIKU chache baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Dk John Magufuli anatarajiwa kuapishwa kesho kutwa (Novemba 5, 2020), kisha kuanza kibarua kizito cha kuunda Baraza la Mawaziri litakaloendeleza kasi ya kaulimbiu yake ya ‘Hapa kazi tu.’ UWAZI linachambua.
Rais Magufuli alikabidhiwa cheti hicho juzi jijini Dodoma na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Semistocles Kaijage baada ya kuibuka mshindi katika mkuu uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 28 nchi nzima huku upande wa Zanzibar ukifanyika kwa muda wa siku mbili (Oktoba 27-28).
Dk. Magufuli alishinda kwa kupata kura milioni 12.5 kati ya kura milioni 15.9 zilizopigwa na kufuatiwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Tundu Lissu aliyepata kura milioni 1.9.
Aidha, licha ya CCM kushinda viti 256 vya ubunge kati ya viti 264, baraza hilo linatarajiwa kujaa sura mpya kutokana idadi kubwa ya wabunge ambao CCM imewapata katika uchaguzi huu.
Katika baraza hilo lenye mawaziri 22, linatarajiwa kutomlazimu Rais Magufuli kuteua wabunge wapya katika nafasi 10 alizonazo kikatiba, hasa ikizingatiwa hata wale mawaziri wa zamani waliokuwa wabunge wa kuteuliwa wameshinda katika majimbo waliyowania kwa mara ya kwanza.
Baadhi ya mawaziri hao walioshinda ubunge kwa mara ya kwanza ni na majimbo yao kwenye mabano ni, Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosa), Dk. Philip Mpango (Buhigwe), Ummy Mwalimu (Tanga Mjini), Prof. Joyce Ndalichako (Kasulu mjini) na Dk. Ashatu Kijaji (Kondoa).
MAONI YA WACHAMBUZI
Akizungumzia Baraza la Mawaziri linalotarajiwa kusheheni ‘sura za kazi’, linalezwa na wachambuzi kusheheni sura mpya za vijana kutokana na uwingi wao ndani ya bunge.
Hoja hiyo inaungwa mkono na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema Rais Magufuli amekuwa kiongozi asiyependa mawaziri wazembe katika baraza lake hivyo upo uwekezakano mkubwa wa kuingiza sura mpya nyingi katika baraza hilo.
“Nadhani Watanzania watarajie mshangao katika uteuzi wake, kwa sababu wabunge 256 ni wengi sana, na asilimia kubwa wanao uwezo mkubwa kiuongozi na elimu toshelevu,” alisema.
Prof. Mpangala alitolea mfano, Mbunge mteule wa Rombo, Prof. Adolf Mkenda na Dk. Charles Kimei (Vunjo) kuwa ni baadhi ya wabunge wanaoweza kukabidhiwa wizara ya viwanda na biashara au fedha na mipango.
Aliongeza, Dk. Kitila Mkumbo (Ubungo) anaweza kupewa wizara ya maji ambayo ameifahamu vema baada ya kuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, wakati Paul Makonda na Mrisho Gambo ni vijana ambao wanaweza kupewa wizara ya mambo ya ndani kutokana na umachachari wao katika usimamizi.
Alisema Tarimba Abbas (Kinondoni) anaweza kupewa wizara ya habari, sanaa, utamaduni na michezo; Fred Lowassa anaweza kupelekwa mifugo na uvuvi wakati Nape Nnauye anaweza kurejeshwa wizara ya habari aliyowahi kuitumikia.
Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya sera na sheria, Mbwana Aliyamtu alisema kwa kuwa Dk. Magufuli hupendelea utendaji wenye kasi na uweledi, sura nyingi za vijana zinatarajiwa kuonekana katika baraza lijalo.
“Kwa sababu katika miaka mitano ya uongozi wake, amebadilisha bazaza zaidi ya mara tano, amewahamisha mawaziri wizara mbalimbali na kuvunja baadhi ya wizara, yote hii ni katika kuboresha utendaji,” alisema.
Aidha, vijana kama Patrobas Katambi, Jerry Slaa na Alexander Mnyeti wanatajwa kuwa na kariba ya uongozi hivyo wanaweza kupewa nafasi za unaibu waziri wa wizara yoyote.
Kwa upande wa wizara ya ulinzi, anatajwa Hamad Masauni kutokana na uzoefu na utulivu wake ndani ya wizara ya mambo ya ndani alipokuwa naibu.
MAWAZIRI ‘VITASA’
Hadi anamaliza muhula wa kwanza wa uongozi wake, Dk. Magufuli alikuwa na wizara 22 licha ya kuanza na wizara 18 alipoingia madarakani Novemba 5, 2015.
Mbali na mabadiliko yaliyotokea katika kipindi chake cha miaka mitano, huku wengine wakitupwa nje, wapo baadhi ya mawaziri waliokuwa ‘vitasa’ kwa kusimama imara katika wizara zao na kumudu kutobadilishwa wala kutupwa nje ya ulingo.
Mawaziri hao sita wasioshikika ni Wiliam Lukuvi, Profesa Joyce Ndalichako, Dk. Philip Mpango, Ummy Mwalimu, Jenista Mhagama na Dk. Hussein Mwinyi ambaye sasa amekuwa Rais wa Zanzibar.
Mawaziri hao pamoja na wengine wa zamani kama vile Dk. Hamis Kigwangala (maliasili na utalii), Dotto Biteko (madini), George Simbachawene (mambo ya ndani), Dk. Godwin Mollel (afya na ustawi wa jamii), Mwigulu Nchemba (katiba na sheri) na Prof. Palamagamba Kabudi (mambo ya nje na ushirikiano kimataifa) wanatajwa kuweza kupewa wizara hizo au kubadilishwa.
Aidha, pamoja na mambo mengine, wachambuzi wa siasa wanaona kuwa upo uwezekano wa kuteua mawaziri wapya kimikoa au kikanda kwa kuzingatia mfumo uliokuwa unatumiwa zaidi na mtangulizi wake Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
MAWAZIRI WALIOANGUKA KURA ZA MAONI
Aidha, baadhi ya wabunge wa majimbo ambao watasubiri huruma ya rais katika nafasi zake 10 za uteuzi wa wabunge ni pamoja na Waziri wa Uwekezaji, Angela Kairuki (Uwekezaji) na aliyekuwa Waziri ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe.
Vigogo hao wote walianguka katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ambapo Kairuki alishindwa na Anne Kilango Malecela katika jimbo la Same Mashariki wakati Mwakyembe akiangushwa na Ally Mlagila ‘Kinanasi’.
HABARI; MWANDISHI WETU
