TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Ijumaa inatarajia kucheza mchezo wake wa tatu wa kuwania kufuzu fainali za mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Tunisia kwenye Uwanja wa Rades, Tunisia kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Stars inashuka katika mchezo huo wa Kundi J huku ikimkosa nahodha wake, Mbwana Samatta anayesumbuliwa na maumivu ya misuli katika mchezo huo dhidi ya vinara wa kundi hilo wanaoongoza wakiwa na pointi sita.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars ambayo iliweka kambi ya muda mfupi nchini Uturuki kabla ya kuelekea Tunisia, Mrundi Etienne Ndayiragije, amesema ana imani na kikosi cha wachezaji wake kuwa watapambana kwenye mchezo huo kupata matokeo mazuri.
“Tunashukuru tumefi ka salama na maandalizi yapo vizuri kwa sababu wachezaji wote ambao tumesafi ri nao wana ari kubwa ya kupambana. Kweli Samatta tutamkosa lakini waliopo huku kila kitu kipo sawa, kitu kikubwa ni Watanzania kutuombea,” alisema Ndayirajige.
Kundi J linaongozwa na Tunisia wakiwa na pointi sita wakifuatiwa na Guinea ya Ikweta yenye pointi tatu, sawa na Libya na Tanzania wanaoshika nafasi ya mwisho katika kundi hilo, ingawa Guinea na Libya zimecheza michezo zaidi. Mchezo wa marudiano utachezwa Novemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
