BONDIA Hassan Mwakinyo anapanda jukwaani usiku wa leo Ijumaa kutetea ubingwa wake wa Mabara wa WBF wa uzito wa Super Welter dhidi ya Jose Carlos Paz wa Argentina.
Pambano hilo la raundi 12 limeandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sport chini ya ukurugenzi na mwanzilishi, Kelvin Twissa na kuthibitishwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa ya Tanzania (TPBRC) na WBF.
Mbali ya pambano hilo, leo pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambapo bondia Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu wa DR Congo ambapo Fatuma Zarika wa Kenya ataonyeshana kazi na Patience Mastara wa Zimbabwe katika pambano la ubingwa wa dunia wa uzito wa super bantam wa WBF na Mtanzania Zulfa Macho atazichapa na Alice Mbewe wa Zambia.
Mbali ya TPBRC, rais wa WBF Howard Goldberg atasimamia pambano hilo huku mwamuzi maarufu duniani, Edward Marshall akiwachezesha mabondia hao ambao wametambiana kila mmoja kushinda pambano hilo.
“Nataka kufanya staili ya mabondia wa zamani kama Mike Tyson ambaye alikuwa anamaliza pambano huku mashabiki wakiwa katika foleni ya kuingia na wengine wakikata tiketi. Nawaomba mashabiki wa ngumi za kulipwa nchini, kuwahi kukata tiketi na kuwahi kuingia ili washuhudie nikiweka historia nyingine,” alisema Mwakinyo.
Paz yeye alisema kuwa mikono yake ndiyo itaongea ulingoni katika kuthibitisha ubora wake. “Najua Mwakinyo anaongea sana, ni kawaida, lakini mimi nitaonyesha vitendo na kuondoka na mkanda huu.”
Twissa alisema tiketi zinaendelea kuuzwa kwa njia ya Nilipe na Selcom kwa Sh milioni 3 kwa meza ya watu 10 na Sh 150,000 kwa kwa viti vya kawaida.
Wilbert Molandi,
Dar es Salaam
