×

Mzimu wa Morrison Waondoka na Kigogo Yanga

BAADA ya kutolewa shutuma za kuihujumu klabu ya Yanga, kamati ya utendaji ya klabu hiyo imefikia uamuzi wa kumsimamisha kazi Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama, Wakili Simon Patrick.

 

 

Jana, Patrick alitoa waraka kukanusha tuhuma zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa anaihujumu timu kwa watani wao Simba SC.

 

Sehemu ya waraka huo Patrick alieleza kusikitishwa kwake na tuhuma za kwamba aliihujumu kesi ya Bernard Morisson kwa Simba: “Mimi ndiye niliyetengeneza ule mkataba, kwa hiyo kisheria nilikuwa sifuzu kutetea ile kesi, hivyo basi klabu iliamua kuweka wabobezi wawili ambao wamenizidi seniority kuweza kupambana na hiyo kesi na ndiyo wanaotuwakilisha huko CAS”.

 

Katika waraka wa kujibu tuhuma zinazomkabili, Patrick amegusia kesi hiyo: “Kesi yetu CAS imesajiliwa kwa namba CAS2020/A/7397. Hii maana yake ni kesi ya 7397. Ikumbukwe CAS inapokea kesi kutoka nchi ambazo ni wanachama wa FIFA dunia nzima, na ina kesi nyingi sana kama ilivyo mahakama ya rufaa ya Tanzania. Hivyo msiwe na haraka sana kwenye masuala ya sheria.

 

“Mpaka sasa Yanga ina kesi nne ambazo Shirikisho limeamua kuzipotezea.  Kesi ya Kabwili, Morisson kuhongwa $5,000 kushawishiwa kuihama Yanga, pingamizi la usajili wa Morrison na kesi ya mkataba wa nyota huyo wa Ghana ambao haujasainiwa na pande zote mbili na nina ushahidi wa kujitosheleza kwamba hizi kesi bado ziko pending kwenye shirikisho letu tukufu.”

Leave a Comment