
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kumwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano wa dharura nchi tatu za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika zinazojulikana kama SADC Organ Troika zikiwa ni Botswana, Malawi na Zimbabwe, ambazo zinazochangia vikosi vya ulinzi na amani vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkutano huo utakaofanyika Novemba 28, 2020, mjini Gaborone, Botswana, utajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda hiyo ya SADC na changamoto mbalimbali zilizojitokeza na namna ya kuzitatua.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa maafisa waandamizi/makatibu wakuu wa asasi ya SADC ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama, Novemba 26, 2020.
Troika ya SADC inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.