
TIMU ya warembo 20 wanaowania taji la Miss Tanzania 2020 leo Novemba 30 lilifanya ziara katika jengo la Global Group lililopo Sinza Mori jijini Dar na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Global Publishers katika kuandaa na kusambaza habari kwa umma na kuwajuza Watanzania kuwa Desemba 5 ndiyo fainali ya Miss Tanzania 2020.
Warembo hao wenye mwonekano wa kuvutia walipokelewa na timu ya wafanyakazi wa Global Publishers kisha kutembezwa kwenye vitengo mbalimbali kama magazeti ya Michezo, Pendwa, Global TV Online, +255 Global Radio, Global App na mitandao yote iliyopo chini ya Global Publishers na kisha wakapata nafasi ya kufanya mahojiano kwenye kipindi cha Katambuga cha Global Radio.

Wakiwa kwenye kipindi hicho walizungumzia Desemba 5, 2020, ambayo waliitaja kuwa ni fainali ya kutafuta mrembo mmoja atakayewakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia ambapo shughuli hiyo itafanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere, (JNIC) uliopo Posta Dar, kuanzia saa 1:00 usiku hadi usiku mnene na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt Tulia Ackson.

Matron wa timu hiyo, Azama Mashenga, akizungumza kupitia Global Radio alisema: “Miss Tanzania 2020, inatarajiwa kufanyika Desemba 5, maandalizi yote yakiwa yamekamilika na Dkt Ackson tunatarajia atakuwa mgeni rasmi. Tunaomba Watanzania waje kwa wingi pale JNIC na viingilio ni rafiki sana, waje waone mapinduzi ya urembo Tanzania kwa mwaka huu maana tunakwenda kuufunga mwaka kibabe.
“Lakini pia tunawashukuru viongozi wa Global kwa kutupa nafasi ya kuja kuzungumza na Watanzania kupitia magazeti, TV na radio, kwani tunaamini jambo letu litawafikia watu wengi zaidi kwa kuwa Global ni kubwa sana,” alisema Masenga.

Akizungumza kwa niaba ya warembo wenzake, Sarafina John, alisema: “Kiukweli tumefurahi kwa mapokezi mazuri mliyotupatia Global, kwa upande wetu tupo tayari kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano ya dunia, kikubwa ni kujiamini, kuomba Mungu na kuwa na ushirikiano ndiyo kitu pekee ambacho kinaweza kutupa taji la dunia. Zaidi tunaoba sapoti ya Watanzania.”
Stori na Issa Liponda.