×

Msalaba Mwekundu Waibuka Kinara wa Huduma Bora Afrika

Wadau wakipasha kabla ya mkutano kuanza.

CHAMA cha Msalaba Mwekundu kimefanikiwa kuwa kinara kwa ubora wa huduma za afya Barani Afrika. Hayo yamesemwa na Rais wa chama hicho, David Mwakiposa kwenye mkutano wa halmashauri kuu ya chama hicho nchini Tanzania ambao umewashirikisha wajumbe na wenyeviti kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, uwakilishi wa vijana, watendaji kazi na watendaji wa chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania.

Amesema kuwa, anawapongeza kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ikiwa ni kutimiza wajibu pale panapokuwa na uhitaji kiasi kwamba imesababisha mpaka kufanya vizuri Afrika na anatarajia watafanya vizuri zaidi kwa Dunia.

“Taasisi ilianzishwa mwaka 1962 nchini Tanzania na sheria ya Bunge namba 71. Ni shirika la kujitolea na huru na lina jukumu la kutekeleza majukumu maalum ya kibinadamu wakati wa majanga, hivyo basi mtu yeyote anayejitolea yupo na sisi.

Rais wa Chama cha Msalaba Mwekundu, David Mwakiposa akizungumza kwenye mkutano huo.

“Tumepiga hatua kubwa, tulikuwa na matawi 30, lakini kwa sasa yapo matawi 1,000 na watu wanaojitolea wamezidi kuongezeka, lakini bado tuna safari ndefu ili ifike mahali kama ndani ya gari inayobeba watu 60 kuwe na watu 6 wa kujitolea na kujua namna ya kuhudumia mgonjwa.

“Kwa sasa tumepata maeneo Tanzania nzima ya kujenga ofisi hivyo tunatarajia ndani ya mwaka mmoja tutakuwa na matawi Tanzania nzima ili iwe rahisi huduma kutolewa kwa wakati.

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli kwa maono ya kupambana na Corona. Pia napenda kuwapongeza wana Msalaba Mwekundu kwa kufanya jitihada kubwa kwa kutoa huduma, lakini ningependa idadi ya vijana iongezeka hata kama endapo kutakuwa na janga; mfano misiba ikitokea hata minne kwa mara moja, basi kila nyumba awepo kijana wa kutoa msaada.

Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, Julius Kejo aliyesimama akizungumza.

“Ni jukumu la vijana kufanya kwa vitendo ili kila shule kuwe na vijana wa kuwapa mafunzo ili panapotokea tatizo wawe wanalitatua na watendaji endeleeni kupambana ili ifike hatua kama kuna eneo lenye uhitaji tulifikie kutoa huduma za maafa, tufikie watoto yatima, masikini wanaoshindwa kupata hata sare za shule tuwahudumie na pengine hata tuweze kwenda nje na Red-Cross inatazama nini tunawahudumia hata wenye magonjwa sugu,” amesema.

Ameendelea kusema kuwa ni lazima kufikiria upya ndani ya miaka minne ijayo wawe wamefika mbali kwa upande wa afya na ameshukuru kwa mapambano waliyoyafanya na kuendelea kutoa huduma kwenye kambi za wakimbizi.

Rais wa Chama hicho, David Mwakiposa akiendelea kusisitiza jambo.

“Tumepambana kukabiliana na  janga la Corona kila mahali tulikuwepo na kutoa huduma na tulifanikiwa hivyo basi niendelee kutoa wito kwa vijana wawe na moyo wa kujitolea ili tuweze kusaidia jamii katika majanga ya aina yoyote ile.

“Shirika la Msalaba Mwekundu tuandae mpango wa miaka mitano ijayo na iwe  na mawazo ya kusambaa nchi nzima hata mtu akiwa amefiwa na mpendwa wake, akikosa jeneza lijue litamsaidiaje,” amesema Mwakiposa.

Naye Katibu Mkuu wa chama hicho, Julius Kejo amesema kuwa watasimamia ajenda ya kufanya kazi ili watoke hapa walipo na kuwa nafasi ya juu zaidi.

Picha ya pamoja baada ya mkutano huo.

“Kama mjuavyo mwaka huu tumekumbana na majanga makubwa ikiwemo mafuriko na ugonjwa wa Corona. Pia tulikuwa na uchaguzi mkuu, lakini sehemu zote hizo tulifanikiwa kutoa huduma, kwa hiyo hayo ni mafanikio makubwa sana kwetu.

“Pamoja na kuwa ni mafanikio tuendelee kufanya kazi kufuata maelekezo kutoka kwa Rais wa chama chetu ili tuweze kuwa na mafanikio zaidi ya haya hata mara kumi yake,” alimaliza kusema Julius.

Leave a Comment