×

Kaze Ampeleka Saido First Eleven Yanga

AKIFANYA mazoezi kwa siku tatu tangu atue hapa nchini kuitumikia Yanga, kiungo mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Said Ntibazonkiza ‘Saido’, ameanza na balaa zito, huku kocha wake, Cedric Kaze akisema ataleta mabadiliko makubwa kikosini akiwa na uwezo wa kumtumia katika mifumo mitatu, 4-5-1, 4-4-2 na 4-3-3.

 

Katikati ya wiki hii, jembe hilo jipya lilitua hapa nchini na kuanza kazi Yanga baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili hivi karibuni.

Nyota huyo raia wa Burundi, tayari ameshaanza mazoezi na wenzake katika kambi yao iliyopo Kigamboni jijini Dar ambapo ameonesha uwezo wa hali ya juu.

 

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, ameliambia Spoti Xtra kuwa, Kaze amevutiwa na uwezo wa nyota huyo baada ya kumuona mazoezini huku akifuata kwa usahihi maelekezo yake.

 

“Ntibazokinza ni miongoni mwa nyota waliofanya mazoezi na timu wakati ilipokuwa ikijiandaa na mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, mwalimu amefurahishwa na uwezo wake, huku akisema ni mchezaji mzuri ambaye ataisaidia timu kwa kushirikiana na wenzake, hivyo ana nafasi kubwa katika kikosi chake,” alisema Bumbuli.

 

Wakati Kaze akiridhika na uwezo wa Saido, beki wa kati wa timu hiyo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amefunguka kuwa: “Kiukweli jamaa ni mchezaji mzuri kutokana na harakati zake ndani ya uwanja kwa sababu anajua kukaa na mpira, kupiga pasi na wakati gani anatakiwa kuwa wapi, ana uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ndani na nje ya eneo la 18.

 

“Naamini atatusaidia pale atakapoanza kucheza rasmi, huyu si mchezaji wa kawaida kwa sababu anajua nini anachofanya, uzoefu wake kwetu ni faida hasa katika kipindi hiki timu inapambania ubingwa.”

KHADIJA MNGWAI NA IBRAHIM MUSSA

Leave a Comment