×

Rekodi ya Caf Yawapa Kiburi Wazimbabwe Mbele ya Simba

MSHAMBULIAJI wa FC Platinum ya Zimbabwe, Mtanzania, Elias Maguli, amefunguka anaamini mchezo wao na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika utakuwa mgumu lakini amekuwa akiamini watabebwa na rekodi yao ya hatua ya awali katika michuano hiyo kufuatia ushindi wa mabao 4-1 katika mechi zao mbili dhidi ya Costal Do Sol.

 

Maguli ametoa kauli hiyo baada ya juzi Jumamosi kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Costal Do Sol ya Msumbiji katika mchezo wa marudiano uliopigwa Harare Zimbabwe ambapo sasa wanatarajiwa kucheza na Simba katika mchezo wa raundi ya kwanza ambao utapigwa Desemba 22-23, mwaka huu nchini kwao kabla ya mchezo wa marudiano Januari 4-5, mwakani jijini Dar.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Maguli alisema kuwa furaha yake kubwa ni kutinga hatua ya pili ya michuano ambapo watakutana na Simba huku akiamini watabebwa na rekodi yao katika michuano hiyo kuweza kusonga mbele tofauti na wapinzani wao.

 

“Kwanza kwangu imekuwa furaha ndoto ya kurejea kucheza nyumbani kwenye michuano mikubwa Afrika nikiwa na timu ya taifa lingine lakini naamini hazitakuwa mechi rahisi zote mbili kwa sababu hata Simba watakuwa wakitaka ushindi wa kuweza kuendelea na michuano hii kama ilivyo kwetu.

 

“Lakini naamini rekodi yetu imekuwa nzuri katika hatua ya awali, tumefuzu kwa ushindi mkubwa wa nje ndani, kitu ambacho kinaongeza hamasa yetu ya kuweza kupata matokeo mazuri katika mechi zote dhidi ya Simba licha ya kwamba halitaweza kuwa jambo rahisi kama inavyochukuliwa,” alisema Maguli.

 IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Leave a Comment