
KIUNGO mshambuliaji mpya wa Yanga, raia wa Burundi, Said Ntibazonkiza ‘Saido’, ametamba kuwa uzoefu alionao kutokana na kufanikiwa kucheza ligi mbalimbali duniani, ikiwemo barani Ulaya, utamsaidia kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Ntibazonkiza alisajiliwa na Yanga baada ya kuonyesha ufundi mkubwa akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Burundi iliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Taifa Stars Oktoba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, huku nyota huyo akifunga bao hilo la pekee dakika ya 86.
Nyota huyo wa zamani wa Vital’O ya Burundi na SM Caen ya Ufaransa, amewahi pia kucheza soka katika nchi za Kazakhstan, Uholanzi na Uturuki.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Ntibazonkiza alisema: “Tangu mwanzo nimeweka wazi kwamba ninayo furaha kubwa kujiunga na kikosi cha Yanga, hasa kutokana na ukubwa wa historia ya klabu hii sio tu kwa Tanzania bali hata Afrika kiujumla.
“Ni jambo zuri kuona tunaongoza msimamo wa ligi mpaka sasa na inadhihirisha juu ya ubora wa kikosi tulichonacho.
“Nimejipanga kushirikiana na wenzangu na kuongeza ule ujuzi nilionao kutokana na uzoefu wa kucheza kwenye ligi mbalimbali, kubwa duniani ili kufanya vizuri na kuisaidia Yanga kufikia malengo yake msimu huu.”
JOEL THOMAS, Dar es Salaam