
RAIS John Magufuli leo Desemba 9, 2020, amewaapisha mawaziri na manaibu wao aliowateua tarehe 5 Desemba 2020, na akawaonya kutotumia magrupu ya kwenye mitandao kuanika siri za utendaji wa kazi zao na za serikali.
Uapisho huo umefanyika leo Jumatano Desemba 9, 2020, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, ikiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambapo pia Rais Magufuli amewakabidhi mwongozo wa Baraza la Mawaziri.
Mawaziri walioapishwa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa. Jumaa Aweso; Waziri wa Maji na naibu wake Maryprisca Mahundi; Kapteni mstaafu, George Mkuchika wa Utawala Bora na naibu wake, Ndejembi John.
Wengine ni Wiliam Lukuvi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na naibu wake, Angelina Mabula; Innocent Bashungwa wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na naibu wake, Abdallah Ulega; na Ummy Mwalimu, Waziri wa Muungano na Mazingira.
Akizungumza wakati wa uapisho huo, Magufuli amesema: “Kazi ya kuwachagua mawaziri na manaibu waziri ilikuwa ngumu, kwani kulikuwa na wabunge zaidi ya 383, na hiyo ndiyo ilikuwa sample yangu huku ukizingatia kuwa wabunge wote hao wana sifa za kuwa Waziri au Naibu Waziri.
“Kazi mliyopewa na majukumu mliyopewa sio mepesi, nendeni mkamtangulize Mungu na Watanzania. Nina matumaini makubwa kwa mliochaguliwa mtakwenda kutekeleza majukumu yenu kwa ukamilifu, msikae sana ofisini, nendeni mkatatue kero za Watanzania. Watanzania wamechoka kusikia maneno Upembuzi Yakinifu (feasibility study) na detailed design.
“Ni nafuu ukafanya uamuzi hata kama ni mbaya kuliko ukawa ‘neutral’ na kutofanya uamuzi; nimewateua mkafanye maamuzi lakini maamuzi mtakayoyafanya yakawe kwa maslahi ya Taifa. Ukifanya kazi itaonekana tu, maana sasa kuna mtindo wa viongozi wa kujipiga picha na kutangaza, jamani hapa ndiyo najiandaa kwenda kukagua miradi, tuache huu ushamba, ukifanya kazi itaonekana.
“Nafahamu kuna magroup ya wakuu wa wilaya, ma-DAS, makatibu wakuu hata watendaji wa kata wana magroup, wakati mwingine nikiiingia humo kuangalia yanayoandikwa, polisi wana magroup yao wanatumiana taarifa na picha za wahalifu. Tujitahidi kutunza siri za serikali.
Wengine walioapishwa ni Jenista Mhagama wa Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu na manaibu wake, Ummy Nderiananga atakayeshughulikia Watu Wenye Ulemavu na Patrobas Katambi wa Kazi, Ajira na Vijana; Profesa Kitila Mkumbo wa Uwekezaji); Dk. Mwigulu Nchemba wa Katiba na Sheria) na Naibu wake, Gefrey Pinda.
Mashimba Ndaki wa Mifungo na Uvuvi na naibu wake; Pauline Gekul; Dk. Damas Ndumbaro wa Maliasili na Utalii na Naibu wake, Mary Masanja; Selemani Jaffo wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi na manaibu wake, Dk. Festo Lugange na David Silinde.
Dk. Medard Kamelani wa Nishati na naibu wake, Stephen Byabato; Profesa Adolf Mkenda wa Kilimo na naibu wake, Husein Bashe; Doto Biteko wa Madini na naibu wake, Ndulane Kumba.
George Simbachawene wa Mambo ya Ndani na naibu wake, Hamis Hamza Hamis; Ummy Mwalimu wa Muungano na Mazingira na naibu wake, Mwita Waitara; Dk. Faustine Ndugulile wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na naibu wake, Kundo Mathew.
Dk. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na naibu wake, Dk. Godwin Mollel. Wengine ni; Dk. Leonard Chamriho wa Ujenzi na Uchukuzi na naibu wake, Msongwe Kasekenya; Geofrey Mwambe wa Viwanda na Biashara) na naibu wake, Kigahe Silaoneka.
Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria; Profesa Joyce Ndalichako ameapishwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na naibu wake, Kipanga Omary.
Manaibu wengine waliapishwa leo ambao mawaziri wao waliteuliwa awali, ni Mwanaidi Ali Hamis wa Fedha na Mipango na William Ole Nasha wa Mambo ya Nje. Mawaziri wa wizara hizo, Dk. Philip Mpango wa Fedha na Mipango na Profesa Palamagamba Kabudi wa Mambo ya Nje, walikwishaapishwa.