
Kampeni za Uchaguzi Mkuu nchini Kenya zinazidi kupamba moto huku zikiwa zimesalia siku chache ili uchaguzi huo ufanyike, ambapo Global TV Online, imefanikiwa kuzungumza na mtangazaji maarufu nchini humo, Robert Ochola (Rowbow) ambaye anagombea udiwani (Member of County Assembly) wa Ziwani Estate, nje kidogo ya Jiji la Nairobi ambaye anafunguka sera zake.
Mwanahabari huyo, anayetumia kauli mbiu ya ‘Hope Unaweza Trust’ kwenye kampenzi za udiwani, ni miongoni mwa wanasiasa wanaopewa nafasi ya juu ya kushinda uchaguzi mkuu, kutokana na jinsi alivyojiweka jirani na jamii yake, hasa eneo la Ziwani ambapo mara kwa mara amekuwa akiwasaidia wananchi wake, hasa maskini.
Miongoni mwa matukio ya upendo yanayombeba Rowbow, ni tukio la hivi karibuni alipoitisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kumsaidia mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa na tatizo la moyo ambapo alitakiwa kufanyiwa upasuaji haraka ili kuokoa maisha yake lakini kwa bahati mbaya, madaktari wote nchini humo wakawa kwenye mgomo, hali iliyotishia uhai wa mtoto huyo.
Akizungumza na Global TV, Rowbow ambaye pia amekuwa mwanaharakati wa muda mrefu wa amani nchini Kenya, ameeleza vipaumbele vyake katika kuwatumikia wananchi endapo atachaguliwa kuwaongoza.