
SIKU ZOTE kuna usemi usemao; “Usililie bahati ya mwe nzako,!” Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwana muziki mdogo, Namite Leasbeth ‘Dinamite’ ambaye asili yake ni mchanganyiko wa Kitanzania na Italia.
Huyu mtoto ameweza kuuchanganya mtima wa msanii mkubwa Afrika Mashariki na sehemu mbalimbali duniani, Nasibu Abdul ‘Diamond’ baada ya msanii huyo kumfuata kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram, jambo ambalo ni adimu sana kwa msanii huyo mwenye wafuasi zaidi ya milioni kumi na moja.
Msanii huyo mdogo mwenye umri wa miaka 13, ambaye ameshatoa nyimbo zipatazo tano, Mazingira, Utamaduni, Happy Day, Tanza-Italia na nyingine, amesema kuwa, ndoto yake kubwa ni kufanya kazi na msanii huyo kwani alianza kuimba na kucheza nyimbo zake tangu akiwa na umri wa miaka mitatu tu, lakini anafurahi zaidi kuona amemsikia na kuonesha kabisa kutaka kutimiza ndoto yake. Ungana na Showbiz ya UWAZI kwa mahojiano yafuatayo;
SHOWBIZ: Habari Namite?
NAMITE: Salama kabisa.
SHOWBIZ: Vipi shule unaendeleaje?
NAMITE: Shule ndiyo tumeanza hivi karibuni maana tumekuwa nyumbani (Italia) muda mrefu kwa sababu ya Corona.
SHOWBIZ: Nimeona kama umetoa wimbo mwingine hivi karibuni, umewezaje sasa katika kipindi cha Corona huko Italia?
NAMITE: Ni wimbo ambao ulikuwepo, sasa nikaona kwa sababu ni muda mrefu niko nyumbani, bora tu niutoe.
SHOWBIZ: Nimeona kwenye mtandao wako wa Instagram, kama Diamond ameku-follow (kuwa miongoni mwa wafuasi wake) kutokana na intavyu yako uliyofanya ya kusema unatamani kufanya naye kolabo, ulijisikiaje?
NAMITE: Kwa kweli nilifurahi sana; yaani hata chakula nilikuwa sihitaji, nilijua wazi kama Diamond ameniona, basi atasikia kilio changu na mimi nitakuwa nimetimiza ndoto yangu.
SHOWBIZ: Kuna wimbo wowote ambao unaujua wa Diamond?
NIMITE: Unajua mimi nimeanza kupenda nyimbo za Diamond tangu nina miaka mitatu na nilianza kuimba vizuri wimbo wake wa Moyo Wangu ambao mpaka sasa ninaupenda sana.
SHOWBIZ: Nyimbo zako unatunga mwenyewe au kuna mtu anakusaidia?
NIMITE: Ninasaidiana na mama yangu, maana yeye ndiye kila kitu kwangu.
SHOWBIZ: Huna mpango wa kufanya kolabo na msanii mwingine?
NAMITE: Wengi tu, lakini nitakuwa ninafanya kwa awamu.
SHOWBIZ: Wimbo wako wa Happy Day, ulifikiria nini hadi ukautunga na kuuimba?
NAMITE: Unajua kila mwanadamu anataka furaha ya kweli, hivyo niliona niwaambie watu ni lazima mtu uwe na siku yako moja ya kufurahi.
SHOWBIZ: Unawezaje kumudu masomo na kuimba?
NAMITE: Kila kitu kipo kwenye ratiba, wala siwezi kuchanganya kabisa.
SHOWBIZ: Video zako nyingi za nyimbo naona, umerekodi hapa nyumbani, hii ikoje?
NAMITE: Ni kweli kabisa, mara nyingi natunga, halafu baada ya muda nikija na mama yangu Tanzania ndiyo ninarekodi video zote.
SHOWBIZ: Naamini kabisa nchi za nje au huko Ulaya kuna studio nzuri na vyombo vya kisasa, kwa nini unapenda kufanyia Tanzania?
NAMITE: Mimi ninapenda nyumbani kwa mama, kwa sababu kuna mazingira mazuri sana, kila kitu ni cha asili ndiyo maana.
SHOWBIZ: Haya asante Namite.
NAMITE: Shukrani sana.
MAKALA: IMELDA MTEMA