
IKIWA ni siku moja baada ya Waziri wa Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleimani Jafo, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Modest Joseph, na kutuma tume ya uchunguzi juu ya ubadhirifu wa fedha za halmashauri hiyo ikiwemo ununuzi wa gari la Tsh milioni 400, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’, ameibuka na iipya tena.
Msukuma amedai kuwa si kisanga cha ununuzi wa gari hilo la Tsh milioni 400 tu, bali Mkurugenzi huyo ametumia kiasi cha Tsh milioni 82 kujenga bustani (garden) huku akiwatimua wafanyabiashara wadogo waliokuwa katika eneo hilo ili atimize azma hiyo.
“Mheshimiwa Rais ametufundisha kubana matumizi ili tuweze kufanya mambo ya msingi na kuwasaidia watu wetu, anakuja mchumia tumbo anachukua pesa za wananchi anatengeza bustani hii, mimi na mbunge mwenzangu Kanyasu na wananchi tumeikataa, nani alimwambia anataka bustani? Kwa nini hiyo pesa asingepeleka kwenye ujenzi wa shule ama barabara, hapa Geita tunapita kwenye tope, barabara hazipitiki.
“Sisi tuliwekwa ndani tukapigwa mabomu sababu ya hizi pesa za GGM, leo hii mtu anakuja kuzichezea sisi hatutakubali, madini haya yataisha lakini lazima kuwe na kitu cha kujivunia kwamba tulifanya, unakwenda na gari la milioni 400 kufungua choo cha Tsh milioni sita kilichojengwa kwa nguvu ya wananchi.
“Ni mara mia angejenga parking (magesho) ya malori siyo huo upuuzi uliofanyika, sisi tunamsapoti Mheshimiwa Rais, watu kama hawa awatumbue tu, na hii garden yake aiondoe hapa hatuitaki maana yake amekiuka maagizo ya waziri mkuu,” amesema Msukuma.
Aidha, Msukuma amempongeza Rais Magufuli kwa kuchukua uamuzi huo huku akisisitiza kuwa bado kuna ubadhirifu mkubwa umefanyika kwenye miradi ya maendeleo mkoani Geita, na hivyo ameomba uchunguzi ufanyike katika miradi yote ya maendeleo inayofanyika mkoani humo.