
POLISI mkoani Kagera inamshikilia Festo Venance mwenye (38) kwa tuhuma za kuwaua watu wawili na kumjeruhi mwingine mmoja, katika kijiji cha Kumzuza wilayani Ngara.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, amewataja waliouawa kuwa ni Magreth Jacob (33) aliyekuwa hawala wa mtuhumiwa, na mtoto mdogo, Jonam Niyonzima, mwenye umri wa miaka mitatu, huku aliyejeruhiwa akitajwa kuwa ni Penina Joseph (40), ambaye amelazwa katika hospitali ya Murgwanza wilayani humo.
Kamanda huyo amesema kuwa sababu ya mauaji hayo bado haijafahamika na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa lakini bado hajakili kuhusika na mauaji hayo, ingawa kuna baadhi ya mazingira yanaonyesha kuhusika kwake, ikiwamo nguo alizokuwa amevaa kukutwa na damu.