×

KMC Watamba Kuwachapa Simba leo

KUELEKEA mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba utakaopigwa leo, kikosi cha Wana Kinondoni, KMC kimejinasibu kuwa wanaimudu Simba na wataibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

 

Mchezo huu utakuwa wa kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu, huku Simba wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yote miwili ya msimu uliopita.

 

Walishinda bao 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa Oktoba 23, mwaka 2019, huku mzunguko wa pili wakiibuka na ushindi wa mabao 3-2 Machi 4, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala alisema wanaiheshimu Simba lakini hawaogopeshwi na ukubwa wa jina lao bali wanaenda kusaka pointi tatu.“

 

Baada ya mapumziko ya siku moja kikosi chetu siku ya Jumapili kilirejea kwenye viwanja vya mazoezi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Simba.“Tunaelekea kwenye mchezo huu tukiwa tumetoka kupoteza mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar jambo ambalo linaweza kuwapa watu hofu.“

Lakini niwahakikishie kuwa tumefanya marekebisho ya makosa yote na tuko tayari kwa vita ya pointi tatu dhidi ya Simba bila kuhofia jina lao, tunawaheshimu na tunaamini kuwa kwa ubora wa wachezaji tulionao na maandalizi yetu tunawamudu Simba na tutapata ushindi,” alisema Mwagala.KMC inakamatia nafasi ya tano kwenye msimamo na pointi zao 21 walizokusanya baada kucheza mechi 13.

Leave a Comment