×

RC Chalamila Asimamia Ubomoaji Nyumba ya Mwananchi

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amesimamia zoezi la kubomoa nyumba ya AtHony Lyuba mkazi wa Kata ya Inyala, Halmshauri ya wilaya ya Mbeya, baada ya kukaidi agizo la kubomoa kwa hiari nyumba yake.

 

Uamuzi wa  Chalamila, ulitokana na Lyuba kukaidi agizo la kupisha mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 16.7, ambao unajegwa kwa kiwango cha lami kuanzia Inyala hadi eneo la Simambwe, ambapo viongozi mbalimbali wa serikali walifika kumtaka avunje nyumba yake kwa hiari lakini aligoma.

 

“Nimeamua nije mwenyewe kubomoa nyumba yako, maana kila wakati tulikuomba kwa hiari yako lakini uligoma, haiwezakani wenzako wote wakubali kubomoa halafu wewe peke yao ugome kama ni imani za kishirikina basi tutaziona,”alisema Chalamila.

 

Mkandarasi wa mradi huo, Imelda Ngailo, amesema kuwa kugoma kubomoa nyumba hiyo kumechelewesha kuendelea na shughuli zingine kwa sababu ya nyumba yake ilikuwa katikati ya hifadhi ya barabara na kwamba mradi huo ulitakiwa ukamilike Desemba mwaka huu (2020) lakini utachelewa kutokana na kikwazo hicho.

 

Lyuba, alikanusha madai ya yeye kugoma kubomoa nyumba na kwamba hakuna kiongozi yeyote alimfuata kumpa maelekezo.

 

“Hakuna Mwenyekiti wa Kijiji wala Kata aliyekuja kwangu kuniambia nibomoe nyumba, zaidi ya kufika ofisini kwako mkuu wa mkoa na nikaamriwa kuwa niko chini ya ulinzi kwa kukaidi agizo la kubomoa kwa hiari nyumba yangu,” alisema Lyuba.

Leave a Comment