
HATARI kubwa! Ndivyo unavyoweza kusema, kufuatia kuongezeka kwa watu wanaofanyiwa upasuaji wa kupandikiza moyo ili kuokoa maisha yao.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba, yamewezesha upasuaji huo mkubwa na mgumu, kuweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa kabisa, rekodi zikionesha kwamba kwa mwaka 2020 pekee, jumla ya watu 3,500 wamepandikizwa moyo duniani kote, nusu ikiwa ni kutoka nchini Marekani ambayo ndiyo inatajwa kuwa kinara wa upasuaji huo.
Akifafanua kwa kina kuhusu upandikizaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mayo – kitengo cha upandikizaji mioyo Marekani, Dk. Eric Steidley, alisema kitaalamu, zoezi la kupandikiza moyo, linaitwa heart transplant au cardiac transplant na zipo aina kadhaa za upasuaji huo, ambapo moyo kutoka kwa mtoaji (donor), hupandikizwa kwa mtu mwenye matatizo sugu ya moyo (recipient) na kuokoa maisha yake.
Dk. Steidley alisema pengine unaweza kujiuliza, ni nani anayeweza kutoa moyo wake na kumpa mwingine. “Inafahamika kwamba moyo ndiyo kama injini ya mwili wa binadamu, unapojitolea moyo, maana yake ni kwamba umekubali kufa kwa ajili ya mtu mwingine, hapo ndipo utata unapoibuka.
“Kwa sheria za mataifa mbalimbali, mtu anayetakiwa kujitolea moyo, anatakiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai wake, kwamba hakuna chochote kinachoweza kumfanya akaendelea kuishi. Watoaji wakubwa wa moyo (donors), ni watu waliopata ajali mbaya au wale waliougua maradhi sugu sambamba na wale wenye tatizo la kufa kwa ubongo (brain death),” alisema.
KINACHOFANYIKA
Aidha, Dk. Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili aliongeza kuwa katika upasuaji huu, mtu anayetakiwa kujitolea moyo, huingizwa katika chumba cha upasuaji na kabla ya upasuaji, madaktari huua ubongo wake (brain death) kwa njia za kitaalamu. Ubongo unapokufa, ni dhahiri kwamba mtu huyo hawezi tena kupona lakini viungo vyake vingine vya mwili vinaendelea kufanya kazi mpaka pale anapokufa kabisa.
“Kwa hiyo, baada ya ubongo kuuliwa, upasuaji hufanyika, moyo hutolewa kutoka kwa mtoaji na kupandikizwa kwa yule mwenye uhitaji.
“Zipo aina mbili za kupandikiza, ya kwanza ni kwamba moyo wenye matatizo kutoka kwa mgonjwa, hutolewa kabisa na kupandikizwa moyo mwingine kutoka kwa mtoaji au kitaalamu ‘orthotopic procedure’ na aina ya pili ni moyo kupandikizwa bila kulazimika kuutoa moyo wenye matatizo, kwa hiyo mgonjwa anabaki na moyo wake wenye matatizo na juu yake ndipo unapopandikizwa moyo mwingine au kitaalamu heterotopic procedure” alisema.
HISTORIA
Aidha, tafiti mbalimbali zinabainisha kuwa licha ya upandikizaji huo kuonekana kama jambo la ajabu sana, upasuaji wa kupandikiza moyo haujaanza jana wala juzi.
Historia inaonesha kwamba majaribio ya awali kabisa, yalihusisha mgonjwa kupandikizwa moyo wa sokwe.
Dk. James Hardy wa Chuo Kikuu cha Mississippi Medical Center ndiye aliyefanya upasuaji huo wa kwanza katika historia, kwa kupandikiza moyo wa sokwe kwenye kifua cha Boyd Rush aliyekuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake kutokana na kusumbuliwa maradhi ya moyo kwa muda mrefu.
Hiyo ilikuwa ni Januari 24, 1964 ambapo Dk. Hardy na timu yake, walifanikiwa kuufanya moyo huo kufanya kazi kwa muda wa dakika 90 na huo ukawa ushahidi kwamba kumbe inawezekana.
Hata hivyo, licha ya moyo huo kuonesha kufanya kazi, hiyo haikuokoa maisha ya mgonjwa huyo lakini ukawa mwanzo wa utafiti mwingine mkubwa kuhusu upasuaji wa aina hiyo.
Majaribio mengine yaliendelea kufanyika na hatimaye, Desemba 3, 1967 binadamu wa kwanza kupandikizwa moyo, alitoka salama kwenye chumba cha upasuaji, akaendelea na maisha na hayo yakawa mapinduzi makubwa katika taaluma ya utabibu wa magonjwa ya moyo.
Upasuaji huo ulifanyika nchini Afrika Kusini ambapo jopo la madaktari bingwa wakiongozwa na Dk. Christiaan Barnard, walimfanyia upasuaji mgonjwa Louis Washkansky katika Hospitali ya Groote Schuur, Cape Town na mgonjwa huyo aliishi na moyo huo kwa siku 18, kabla ya kupata ugonjwa mwingine wa nimonia ambao ndiyo uliokatisha maisha yake.
Mafanikio hayo, yaliwapa morali madaktari wengi zaidi duniani na inaelezwa kwamba ndani ya mwaka huo, oparesheni zaidi ya 100 za kupandikiza moyo zilifanyika, ingawa ni theluthi moja tu ya wagonjwa ndiyo walioendelea kuishi.
Inaelezwa kwamba kitaalamu mtu aliyepandikizwa moyo, anao uwezo wa kuishi mpaka miaka 15 tangu siku alipofanyiwa upasuaji huo
Changamoto kubwa ya watu wanaopandikizwa moyo, kama ilivyo kwa watu wanaopandikizwa viungo vingine ndani ya miili yao, ni kinga ya mwili kupambana na kiungo kilichopandikizwa, jambo ambalo kitaalamu huitwa ‘rejection’.
Ugunduzi wa dawa iitwayo Cyclosporine mwaka 1983, ulikuja kutatua changamoto hii ambapo sasa baada ya kupandikizwa moyo, mgonjwa alikuwa akilazimika kuendelea kutumia dawa hizi ili kuzuia kinga ya mwili isiudhuru moyo uliopandikizwa.

BIASHARA HARAMU
Mfumo wa maisha hasa katika nchi zilizoendelea, umesababisha watu wengi kukumbwa na matatizo ya moyo na hivyo, uhitaji wa kufanyika kwa oparesheni za kupandikiza moyo umeongezeka kuliko kawaida.
Kwa mwaka 2020 pekee, kama ilivyoelezwa, watu zaidi ya 3,500 wamefanyiwa upasuaji huo kwa mafanikio makubwa lakini ipo idadi kubwa ya wagonjwa ambao wanasubiri kupandikizwa moyo, changamoto iliyopo ni kwamba watu wa kujitolea moyo hawapatikani kwa urahisi.
Hiyo imesababisha wahalifu kuitumia fursa hiyo, ambapo biashara ya usafirishaji wa binadamu inayopingwa vikali na jumuiya mbalimbali zikiwemo Umoja wa Mataifa, imezidi kushamiri.
Watu wanarubuniwa kutoka katika nchi maskini, kwamba wanaenda kutafutiwa ajira Ulaya lakini wakifika huko, huuawa na mioyo yao kuuzwa kwa ‘matajiri’ wenye matatizo ya moyo.
Licha ya mataifa mbalimbali kuwa na sheria kali zinazoeleza ni nani anayeruhusiwa kisheria kutoa moyo wake kumpa mwingine, kasi ya biashara ya binadamu inazidi kushamiri duniani kote na kusababisha kuwe na kazi ya ziada ya kudhibiti biashara hiyo haramu.
JKCI NAO MBIO KUPANDIKIZA MIOYO
Wakati Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ikiendelea kuboresha huduma zake, imeelezwa kuwa inajiandaa kuanza matibabu ya upandikizaji wa moyo kwa wagonjwa.
Akizungumza na UWAZI kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi alisema zoezi hilo la upandikizaji lipo kwenye mpango wa muda mrefu wa taasisi hiyo.
“Hili sio zoezi la kusema leo, na kuanza ukaanza kupandikisha, linahitaji rasilimali kubwa… kwa hiyo ni mpango wa muda mrefu, kuanzia miaka mitano ndio taasisi yetu inaweza kuanza kutekeleza zoezi hilo,” alisema.
Aidha, Januari mwaka huu akizungumzia mafanikio ya miaka minne ya taasisi hiyo Profesa Janabi alisema watalaam katika nchi zilizoendelea duniani wameanza kutengeneza artificial heart (moyo bandia).
Alisema sio lazima kupata mfadhili wa moyo kwa sababu upo uwezekano wa kutengeneza vitu vinavyofanana na moyo wa binadamu.
“Hivyo sisi kabla hatujafika huko kutengeneza moyo bandia, tupo mbioni kuanza upandikizaji huu wa moyo kutoka kwa mfadhili, sio oparesheni kubwa,” alisema Janabi.
Hata hivyo, Janabi alisema changamoto kubwa ya upandikizaji wa moyo ni kupata idhini kwa mgonjwa, ambaye yupo taabani na matibabu yameshindikana na kuna kila dalili akapoteza maisha, hivyo atatakiwa kuridhia ili moyo wake utolewe na awekewe mgonjwa.
“Kupata moyo kwa ajili ya kupandikiza, inaweza kuwa ngumu. Moyo ni lazima utolewe kwa mfadhili (donor) ambaye ubongo wake umekoma kufanya kazi, lakini moyo huo unatakiwa kuwa na uwezo wa kuendeleza maisha ya mpokeaji.
“Japan pamoja na maendeleo yao yote, upandikizaji wa moyo upo nyuma, ni kwa vile imani yao ni buddhist, hawaamini kutoa kiungo cha binadamu mmoja kwenda kwa mwingine, maana ili uweze kupandikiza moyo mtu kabla hajafa, lazima upate idhini yupo tayari kutoa moyo kwa mgonjwa, “alisema.
Aliongeza: “Ukiondoa watu wanaopata ajali hapa kwetu ambao hufanyiwa postmortem bila idhini kutokana na hali zao, sasa hivi tuna changamoto ya ndugu wachache ambao wanaweza kuwa tayari mgonjwa kufanyiwa postmortem ili kujua kitu gani kilifanya mgonjwa afariki kisha kutolewa moyo, hili linahitaji uelewa mpana kwa siku zijazo”.
Alisema wao kama taasisi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wanasiasa na watunga sera, wana jukumu la kuelimisha jamii kuhusu suala hilo.
“Sisi kama taasisi na wizara tuanze kuelimisha jamii, maana moyo lazima upatikane ambao bado unadunda. Kama tunataka kuelekea huko lazima tuanze kutoa elimu kuanzia sasa,”alisema Janabi.
Kwa mujibu wa Mtandao wa https://medlineplus. gov/hearttransplantationunaeleza kuwa moyo unaopandikizwa, ambao utatoka kwa mfadhili, lazima ufanane kwa kadri iwezekanavyo na aina ya tishu za mpokeaji ili kupunguza uwezekano wa mwili kuukataa.
Mtandao huo unaeleza kuwa kumekuwa na matukio 171 ya upandikizaji wa moyo katika kipindi cha miaka 12 iliyopita nchini Uingereza.
HABARI; MWANDISHI WETU, UWAZI