×

Wasauz Wamrudisha Dube Uwanjani

MADAKTARIwaliosimamia matibabu ya straika hatari wa Azam, Prince Dube kutokea nchini Afrika Kusini ‘Sauz’, wamempunguzia straika huyo muda wa kukaa nje ya uwanja, kutoka wiki nne hadi sita zilizotajwa hapo awali mpaka wiki tatu.

 

Dube, mwenye mabao sita na asisti nne mpaka sasa, alivunjika mkono Novemba 25, mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Yanga hali iliyosababisha apelekwe Afrika Kusini kwa matibabu, Novemba 29, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’, alisema kasi ya uponaji wa jeraha la nyota huyo, imekuwa ya kuridhisha, na madaktari wake wanaamini ndani ya muda huo wa wiki tatu, Dube atakuwa tayari kuanza mazoezi.“

 

Habari njema kwa mashabiki na wadau wa Klabu ya Azam ni kwamba, nyota wetu raia wa Zimbabwe, Prince Dube, anatarajiwa kurejea uwanjani mapema zaidi kuliko ilivyoelezwa hapo mwanzo.“

 

Ambapo tuliambiwa angekaa nje kwa wiki nne hadi sita lakini madaktari wake kutoka Afrika Kusini wametuambia nyota huyo atakaa nje kwa muda mchache zaidi wa wiki tatu pekee.“

 

Na tayari nyota huyo amepatiwa programu maalumu ya kuweza kumrudishia kasi kwa kuwa unapokuwa na jeraha la mkono, sehemu kubwa ya mwili wako bado inakuwa kwenye nafasi ya kufanya kazi hivyo ataendelea na programu hizo hadi pale kila kitu kitakapokuwa sawa,” alisema Thabith.

 

Sare waliyoipata Azam Jumamosi dhidi ya Namungo imewafanya wafikishe pointi 28 zinazowaweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo baada ya kucheza mechi 15 mpaka sasa.

Stori: Joel Thomas,Dar es Salaam

Leave a Comment