×

Dimpoz Hakamatiki Kimataifa!

MSANII wa Bongo Fleva, Omari Nyembo almaarufu kwa jina la ‘Ommy Dimpoz’ anazidi kuchanja mbuga kimataifa baada ya kusaini mkataba mpya wa kibiashara na kampuni ya muziki, Sony Music Entertainment Africa ya jijini Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

 

Tukio hili la kusaini mkataba huo lilifanyika mapema mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo hapo Ommy anathibitishia ulimwengu wa burudani kuwa yeye ni moto wa kuotea mbali kimataifa.

Dimpoz alithibitisha kujiunga na kampuni hiyo huku akisema

“Ni fahari kwangu kujiunga na Sony Music Entertainment. Nitazidi kuonyesha makali yangu kila uchwao.”

 

HATUA KIMATAIFA

Katika kile kinachoonekana kuwa Ommy amejipanga vilivyo kufanya kazi anga za kimataifa, mapema Desemba 10, mwaka huu, aliachia singo yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Dede’.

Singo hiyo aliyoshirikiana na wasanii wa kimataifa wa nchini Afrika Kusini, ni mwanzo wa kuelekea kuachia albamu yake mpya itakayotoka siku za usoni.

Mastaa walioshirikiana na Ommy katika ‘Dede’ ni pamoja na Dj Tira, Dladla Mshunqisi na Prince Bulo.

 

KAULI YA OMMY

Akizungumzia shavu hilo, Ommy Dimpoz anasema, “Nimefurahi kujiunga na Sony, nyumba ya wasanii wenye vipaji duniani, ushirikiano huu ni hatua muhimu sana kwenye muziki wangu na umekuja wakati sahihi kwenye maisha yangu.

 

“Najua wasanii tupo wengi… unapoona unakubalika kuingia kwenye kampuni kubwa ya kimataifa kama hii, basi ni dhamana kubwa. Nami nawaahidi kwa dhati mashabiki wangu kwamba nitafanya kazi nzuri, sitawaangusha kabisa. Nitawafurahisha.”

 

Katika kuonyesha alivyojipanga kutoa burudani ya kiwango cha juu kwa mashabiki wake, Ommy Dimpoz alisema kuwa album yake mpya ambayo ndani yake kuna singo ya ‘Dede’ itaachiwa hewani mapema mwakani, ikiwa chini ya ushirikiano wake na Kampuni ya Sony Music Entertainment Africa.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Sony Music Entertainment Africa, Sean Watson anasema: “Tunajivunia sana kuwa na msanii wa kiwango cha Ommy Dimpoz, tumefurahi sana Ommy kufanya uamuzi wa kushirikiana nasi

Tunafurahi kuungana naye kuleta muziki wake mzuri na wa kushangaza masikioni mwa mashabiki wengi kadiri tuwezavyo.”

 

ALIPOTOKA OMMY

Awali, Ommy Dimpoz alianza muziki kama mwimbaji wa bendi ya msanii wa Kibongo, Khaleed Mohamed T.I.D kabla ya baadaye kuibuka kama mwanamuziki wa kujitegemea na wimbo wake wa kwanza ukawa ni ‘Nai Nai’ akiwa amepiga kolabo na Alikiba.

T.I.D ni kama alimfungulia milango ya muziki, kwani baadaye alitoka na kibao ‘Mama’ akiwa ameshirikiana na msanii mkali wa Bongo Dansi, Christian Bella.

 

‘Me and You’ wimbo alioshirikiana na msanii Vanessa Mdee ukamtambulisha ndani ya mipaka ya Afrika Mashariki na hapo ndipo Ommy alipoendelea kuwasha moto kwenye ulimwengu wa muziki.

Vibao vyake vingine ni pamoja na Hello Baby aliomshirikisha msanii Avril kutoka Kenya, Achia Body, Tupogo, Wanjera, Ndagushima na Kajiandae.

 

Mwaka 2017, Ommy Dimpoz alijiunga na Lebo ya muziki ya Rockstar Africa Record ambapo aliungana na msanii Alikiba na wasanii wengine katika lebo hiyo.

Akiwa kwenye lebo hiyo, alipata nafasi ya kufanya kazi na msanii wa Kinigeria, Deborah Oluwaseyi Joshua almaarufu kwa jina la Seyi katika wimbo uitwao ‘Wanje’ lakini baadaye akapatwa na tatizo la kiafya.

 

Alianza kupatiwa matibabu hapa nchini kabla ya baadaye kupelekwa Kenya ambapo alionekana kuwa na tatizo lililohitaji kufanyiwa upasuaji haraka.

Alidumu katika matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima ndipo aliporejea hadharani akiwa mzima wa afya njema baada ya kupatiwa matibabu ya kina.

 

Ni hapo Ommy Dimpoz alipomshukuru Mungu kwa uponyaji wake kwa kuachia wimbo ‘Baba Ni Wewe’ ambao ulikuwa maalum kwa Mungu – kwa kumsimamia kwenye matibabu yake.

Nyimbo nyingine zilizofuata baada ya huo zilikuwa ni ‘One and Only’ alioshirikiana na Petra, ‘Show Me’, ‘You’re The Best’, ‘Hello’ alioshirikisha Mwana-FA na ‘Kata’ aliomshirikisha staa wa kike kwenye Bongo Fleva, Nandy.

Leave a Comment