
MBUNGE mstaafu Susan Lyimo, leo amewanoa madiwani wanawake kutoka katika halmashauri 24 ambazo ni mikoa 9 wanaoendelea na mafunzo ya malezi ya uongozi bora kwenye ofisi za Mtandao wa Jinsia (TGNP) zilizopo Mabibo Jijini Dar.
Akitoa mafunzo kwa hayo kwa madiwani hao waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita Susan ambaye kitaaluma ni mwalimu wa sekondari na mwanasiasa aliwafundisha namna mbalimbali za kukabiliana changamoto za uongozi kwa mwanamke na kujitolea mifano yeye mwenyewe jinsi alivyokabiliana nazo na jinsi alivyozitatua kiuzoefu.

Suzan aliwakumbushia madiwani hao harakati zake za kutetea wanawake tangu alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichopo Mlimani (UDSM)
Wakati akitoa mafunzo hayo wakati mwingine alikuwa akitumia mtindo wa kupokea maswali ambapo baadhi ya madiwanio hao walimuelezea jinsi mfumo dume unavyowapa hofu kwenye baadhi ya jamii.

Suzan aliwatoa hofu ya mfumo dume na kuwataka kujiamini akiwaambia kuwa mambo ya kuhofia mfumo dume yalishapitwa na wakati.

Akielezea jinsi ya kutimiza ahadi za wananchi Suzan aliwaambia wanachotakiwa ni kuorodhesha shida za wananchi wao na kuwauliza waanze na lipi na litakalotajwa ndiyo linalotakiwa kuanzwa nalo kwa maana wakati mwingine mahitaji yanaweza kuwa mengi na kuwa vigumu kutekelezeka yote kwa kipindi utakachokuwa madarakani.

Wengine waliotoa mafunzo kwa madiwani hao ni pamoja na mwezeshaji mzoefu wa masuala ya uongozi, Geofrey Chambua na Mratibu Mwandamizi wa Mafunzo hayo, Jane Tesha.

Mafunzo hayo yanaendelea kwenye ofisi hizo ambapo wanawake hao wamedhamiria kufikia asilimia hamsini kwa hamsini za uongozi na wanaume. HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS GPL